Na Zaka Zakazi
Kibaden Shujaa wa mabao matatu (hat trick hero) kwenye mapambano ya watani wa jadi, Abdallah Athuman Seif almaarufu Abdallah Kibaden au King Mputa, amesema hakushangazwa kuona bao ‘halali’ la Ibrahim Ajib likikataliwa na mwamuzi Martin Saanya aliyepotoshwa na mshika kibendera wake, Ferdinand Chacha, kwenye pambano la watani wa jadi Oktoba Mosi mwaka huu.
Kibaden ambaye historia inamtambua kama binadamu pekee kuwahi kufunga mabao matatu kwenye mchezo mmoja wa Yanga na Simba, anasema hata kwenye mchezo ambao yeye alifunga mabao matatu, refa alikataa moja ya mabao yao.
“Mwaka 1977, sisi Simba tuliwafunga Yanga 6-0, mimi nikifunga mabao matatu. Wakati tunaongoza 3-0, Athuman Juma (marehemu) alipiga mkwaju wa adhabu ndogo kutoka katikati ya uwanja, mpira ukaingia wavuni lakini refa akalikataa bao hilo,” anasema Kibaden huku akitikisa kichwa.
“Siku ile tungewafunga Yanga mabao 7, lakini refa akatunyima bao letu halali,” anasema Kibaden ambaye jina hilo alipewa na watoto wenzake enzi za madrasa. Hapo Kibaden alikuwa anaizungumzia mechi ya Julai 19, 1977, inayobaki kuwa mechi ya kipigo kikubwa zaidi kwa watani wa jadi. Kibaden alifunga mabao yake dk. 10, 42 na 89. Mabao mengine yalifungwa na Jumanne Hassan ‘Masimenti’ aliyefunga mawili dk. 60 na 73 na bao lilikuwa la kujifunga la Selemani Sanga dk. 20.
Akiizungumzia siri ya ushindi ule, Kibaden anasema wachezaji wa Simba walikuwa wanalipa kisasi kwa wachezaji na mashabiki wa Yanga waliowazomea siku chache kabla ya mchezo huo.
“Kabla ya mechi yetu ambayo ilifanyika mwishoni mwa juma, kulikuwa na mechi kati ya Yanga na timu moja ambayo nimeisahau. Ilikuwa siku ya Jumatatu au Jumanne, sisi wachezaji wa Simba tulikuwa kambini Kibaha, lakini siku hiyo tuliacha kufanya mazoezi tukaenda kuwatazama Yanga, wakashinda mabao 4-0. Mwisho wa mchezo mashabiki wao wakaanza kutuzomea na kuturushia maganda ya machungwa huku wakisema zamu yetu inakuja”, anakumbuka Kibaden.
“Tuliporudi kambini kwetu Kibaha, tukamuomba kocha wetu, Tamsarov kutoka Bulgaria, atuache tukafanye mazoezi usiku badala ya kulala. Uwanja haukuwa na taa hivyo tuliwasha taa za magari machache yaliyokuwepo ili kuzalisha mwanga.”
Siku ya mechi, Yanga hawakuamini kilichowatokea. ‘Tuliwashambulia tangu filimbi ya kwanza. Dakika ya 10, mimi nilipata mpira katikati, nikakimbia nao na kuwapiga chenga watu watatu na kufunga kwenye goli la Kaskazini. Willy Mwaijibe (marehemu) akafunga bao la pili. Mimi nikafunga bao la tatu. Ilipigwa kona ndogo na Athuman Juma (marehemu) nikaunganisha moja kwa moja. Tukaenda mapumziko tukiongoza 3-0. Kipindi cha pili ndiyo refa akatukatalia bao letu halali.
Hata hivyo, mvua ya mabao ikaendelea kuwanyeshea Yanga na Jumanne Hassan ‘Masimenti (marehemu) akafunga mabao mawili. Kutokana na mashambulizi makali, Selemani Sanga wa Yanga akajifunga bao na dakika za mwisho nikafunga bao langu la tatu na la sita kwa timu yetu. Abbas Dilunga alikimbia na mpira upande wa kushoto, akapiga krosi mimi nikamalizia.