Image captionMamba aliyepewa jina Big Daddy (kulia) na wenzake
Mmoja ya mamba wakubwa zaidi duniani kwa jina Big Daddy, ambaye anafugwa katika katika Mamba Village, mjini Mombasa, atafungishwa ndoa rasmi na wake zake wawili, Salma na Sasha.
Hafla hiyo ya kipekee inatarajiwa kufanyika Aprili tarehe 29 mwakani mjini Mombasa.
Mamba huyo ana uzani wa tani moja na anaaminika kuwa na umri wa zaidi ya miaka 100.
Image captionBig Daddy alianza kuishi Mamba Village mwaka 1986
Waandalizi wa ndoa hiyo wanasema wameamua kumsaidia Big Daddy afanye harusi baada ya kuwapa wake zake wawili penzi motomoto kwa miaka 30.
Alikuwa amewekewa mamba wengine wawili aishi nao lakini akawala.
David Mbatu, mmoja wa wahudumuwa Mamba Village wanaosaidia kuandaa harusi hiyo anasema keki ya harusi itakuwa ni mfupa wenye mnofu wa nyama na damu.
"Big Daddy alikuja hapa mwaka 1986 tukamchagulia wake wanne, akaua wake wawili akabaki na hawa wawili. Sasa amekuwa na hao wawili kwa miaka 30. Sasa kama ameonyesha upendo wa miaka hiyo basi tuonyeshe mfano pia mamba anaweza akafanyiwa ndoa," anasema.
Image captionMamba Village
Mipango ya awali ilikuwa harusi ifanyike mwezi Desemba lakini baadaye wakakumbuka kwamba kipindi hicho mamba huwa wana mayai.
"Hajajua. Atajua tu siku hiyo, kwa sababu tutafanya mazoezi kumuonyesha kwamba kuna kitu fulani kitakuja. Wajua mamba ana kumbukumbu nzuri sana."
Kwa vile hawawezi kuwavalisha mamba hao nguo za harusi, watajaribu kuwapamba.
Maimuna Siraj pia ni miongoni mwa wanaopanga harusi hiyo.
"Ukiangalia mapenzi yao yanavutia, mara wenyewe wanakumbatiana, wanapigana busu. Na ukiangalia ni sehemu moja. Kama ni mtu mwingine, angetengea nyumba mbalimbali au boma kando kando."
Image captionMaimuna anasema zamani Big Daddy alikuwa na ukali kupita kiasi
"Kabla apate hawa mamba, alikuwa anawala mamba wengine. Lakini hawa wanawake wameweza kumtuliza."
Sasha alitoka bara lakini Salma asili yake ni pwani.
Image captionMamba wengi watakuwa wamebeba mayai mwezi Desemba
Paul Mutua, meneja wa bidhaa wa Mamba Village, watalii na wageni mashuhuri wanatarajiwa kufika kushuhudia harusi hiyo.
Anasema wanapanga kumwalika waziri wa utalii Najib Balala na hata Rais Uhuru Kenyatta.
"Tutakuwa na watalii kutoka humu nchini na tunatarajiwa wageni hata kutoka nje ya nchi," anasema.