Na Baraka Mbolembole
MICHEZO yake mitano ya mwanzo klabuni Simba SC, mlinzi wa kati, Mzimbabwe, Method Mwanjali ameonekana kuwa beki mtulivu, anayeweza kujipanga vizuri na kuupanga ukuta wote. Ameonekana ni mchezaji mzuri wa mwisho na maamuzi yake yamekuwa na faida.
Mwanjali ikiwa amebaki pekee dhidi ya mshambuliaji wa timu pinzani anakuwa na maamuzi sahihi. Atajitahidi kwa namna yoyote kuucheza mpira lakini uwezekano huo ukikwama atamzuia kwa ‘faulo ya kitaalamu’ mpinzani wake ili asiweze kupeleka madhara golini kwao.
Ndivyo beki wa kati anavyotakiwa kucheza. Katika game iliyopita vs Azam FC, mechi ambayo Simba walishinda 1-0, beki huyo wa kati alionekana kucheza vizuri na kijana, Novatus Lufunga na kama walifanya makosa basi ni machache.
Hadi sasa ‘kibabu’ huyu ameonekana ni mchezaji mzuri, mlinzi wa kati asiye na makosa mengi. Lakini tatizo la kukosa kasi linaweza kuleta picha tofauti kuhusu uwezo wake. Kucheza na mshambulizi ‘taipu’ ya Donald Ngoma si sawa na John Bocco.
Nahodha huyo wa Azam FC, Bocco anafahamika kwa kutokuwa na kasi, Bocco pia hana ufundi mwingi ila ni mshambuliaji mwenye shabaha na nguvu anapokuwa uwanjani.
Mwanjali atapata wakati mgumu dhidi ya wachezaji wenye kasi lakini katika VPL huenda tatizo hilo lisimuathiri kwa kuwa ukiwatoa washambuliaji wa Yanga ni timu chache sana zenye kufanya mashambulizi ya kasi.
Hivyo, Mwanjali atakuwa na nafasi ya kuendelea kucheza kama mlinzi bora wa kati kulingana na wapinzani anaokutana nao.
Ana mwili mkubwa, umri wake ni zaidi ya miaka 33, anajua kujipanga, ana uwezo wa kufika vizuri kwenye mpira na kuupora kutoka kwa mchezaji wa timu pinzani. Hadi sasa amefanya vyema na anapaswa kusifiwa kwa kuifanya beki ya Simba kuwa na utulivu huku wakihakiki vizuri mpira.
Kwa jinsi alivyo na kasi ndogo, Mzimbabwe huyu anategemea kuwakumbusha wenzake mara kwa mara ili kusiwepo na umbali kati yao na washambuliaji wa timu pinzani.
Kiasi nimevutiwa na namna anavyookota mipira, anavyoipanga beki yake, anavyohakiki kwa umakini na vile anavyoiondoa timu yake nyuma kwenda mbele, ila kuhusu kasi yake, bado atasumbuliwa sana na safu ya mashambulizi ya Yanga ambayo ina kasi, nguvu na shabaha ya kufunga magoli.
Hadi sasa ‘kibabu’ huyu ameonekana kuwa beki mzuri ila ubora wake bado hauwezi kupimwa na safu za mashambulizi za Ndanda FC, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, au Azam FC ambazo hazina kasi.
Nadhani vs Ngoma, Tambwe, Msuva, itakuwa tofauti. Nasikia katika ligi kuu ya Afrika Kusini alikuwa kinara wa kutoa ‘maboko’ ila hadi sasa sijaona makosa yake, zaidi ya kasi yake, kibabu huyu amefanya vizuri hadi sasa.
Simba imeruhusu magoli mawili tu katika game tano za VPL ni takwimu nzuri kwa safu ya ulinzi kwa maana waliisaidia timu kupata alama moja siku ambayo washambuliaji hawakufunga dhidi ya JKT Ruvu. Mtibwa Sugar hawakufunga goli na imekuwa hivyo pia dhidi ya Azam FC.
Siwezi kusema wao ni bora kupita kiasi ila hadi sasa wana umakini mkubwa na uongozi wa Mwanjali umekuwa na faida kwa maana umejenga utulivu hadi kwa kijana Lufunga.