Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika kipindi kingine cha Ijue Afya Yako. Katika kuhitimisha kujadili maradhi ya ngozi leo tunaangalia maradhi ya fangasi ya mapunye yanayoshambulia kichwa ambayo kitaalamu huitwa Tinea capitis.
Aina hii ya maradhi ya fangasi hushambulia eneo la kichwa pekee ukiacha eneo la uso. Kwa maneno mengine, aina hii ya fangasi haishambulii uso bali eneo lililobaki la kichwa. Lakini je, mapunje huwashambulia kina nani zaidi? Ugonjwa huu hushambulia watu wote wa jinsia na umri wote, ingawa huonekana zaidi kwa watoto wadogo. Fangasi hawa hushambulia watoto wadogo ambao hawajafikia umri wa balehe na mara nyingi huacha kushambulia pale mtoto anapofikia umri huo wa balehe. Iwapo unataka kujua muonekano wa maradhi haya, unapaswa kujua kuwa, mapunye huweza kushambulia eneo zima la kichwa au sehemu tu ya kichwa. Eneo la ngozi ambalo lina mashambulizi ya mapunye huwa na umbo linalofanana na sarafu. Eneo hili la ngozi lililoathirika kama lina nywele, hunyonyoka na hivyo mwonekano wa mfano wa sarafu huonekana wazi hata bila kutumia jicho la kitaalamu.
Dalili zake
Ukiachilia mbali mwonekano wa mapunye kama tulivyoeleza kuna dalili nyingine za maradhi haya ambazo ni: Eneo la ngozi lililoshambuliwa kuwasha, ingawa si mara zote na kubadilika kwa rangi ya ngozi ya eneo lenye maambukizi. Ukitazama kwa makini eneo ambalo lina mashambulizi ya maradhi haya utagundua kuna vidoti vyeusi ambavyo vinaonyesha eneo ambalo nywele imeng'oka kutokana na maradhi. Dalili nyingine ya mapunye ni ngozi kubanduka kwenye eneo lenye maambukizi na pia ngozi kukauka kwenye eneo hilo. Mara nyingine usaha pia huweza kuonekana kwenye eneo la ngozi lililoshambuliwa na fangasi hawa na hali hiyo kitaalamu huitwa kerions. Kama maradhi haya yakikaa bila kutibiwa kwa muda mrefu husababisha dalili nyingine ambayo ni kuonekana kama kutoka majimaji kwenye eneo la ngozi lililoathirika pamoja na kutoka harufu mbaya kwenye eneo hilo lililoathiriwa na vimelea hivi vya fangasi. Kuna njia nyingi zinazoweza kusababisha uambukizi wa mapunye lakini ili uambukizaji huu uwezekane lazima kuwe na mazingira yanayofaa ya kuwezesha fangasi kuishi na kuhama kwa urahisi. Mazingira haya yanayofaa kuruhusu fangasi hawa kuweza kutoka kwenye kichwa cha mtu mmoja kwenda kwa mwingine huhitaji uwepo wa hali ya joto pamoja na majimaji au unyevunyevu. Watu ambao wako katika hatari ya kupata maambukizi ya mapunyeni ni wale wanaoshirikiana na wenzao vifaa vya kunyolea bila kuvisafisha vizuri na pia wanaoshirikiana vifaa vya kufanya usafi wa mwili zikiwamo taulo. Vilevile wanaotoka jasho sana hasa kichwani kwani huweza kuweka mazingira mazuri zaidi ya kuruhusu maambukizi ya ugonjwa huo yatokee kirahisi. Wale wanaofanya kazi zinazohusisha uwekaji vichwa kwenye maji yaliyotuama kwa muda mrefu na wale ambao tayari wana fangasi za kichwani kwani ni rahisi kwa fangasi hao kujirudia. Kundi jingine lililo katika hatari ya kupata ugonjwa wa Tinea capitis ni na wale watu wanaofanya usafi wa mwili kwa kutumia maji yaliyobeba vimelea vya fangasi wa mapunye, wasiojikausha vichwa baada ya kuoga au kutofanya usafi wa kichwa kwa ujumla na watu wenye maradhi yanayosababisha kushuka kwa kinga ya mwili kikiwemo kisukari. Hali kadhalika wale wanaokunywa kwa muda mrefu dawa za kuua vimelea yaani antibiotiki na pia watoto wadogo ambao hawajafikia umri wa balehe.
&&&&&&&&&&&&&&&&&&
Huwa ni rahisi sana kwa mapunye kuambukizwa kutoka kwenye kichwa cha mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia zifuatazo. Moja ni kutumia vifaa vya kunyolea kwa zaidi ya mtu mmoja bila kuvifanyia usafi wa kuua vimelea kama fangasi wa aina hii. Pili kutumia taulo au nguo ya kujikaushia kwa mtu zaidi ya mmoja hasa pale ambapo mmoja wa watumiaji hao ana maambukizi haya ya fangasi. Kutumia vifaa vya nywele kama chanuo la kuchania nywele kwa zaidi ya mtu mmoja hususan pale ambapo mmoja wa watumiaji hao ana maambukizi ya vimelea vya fangasi hawa, kugusana na mtu aliye na maambukizi tayari na pia kushirikiana mavazi aina ya kofia na mtu aliyekwisha pata maambukizi hayo.
Kuhusiana na kuutambua ugonjwa huo mara nyingi aina hii ya fangasi hugundulika kwa macho hasa kwenye maeneo ambayo fangasi hao wapo kwa wingi. Kwa kutazama ngozi ya sehemu ya kichwa iliyoathirika na maambukizi ya fangasi hao, utaweza kuona madhara yanayokukabili. Iwapo vipimo vitahitajika basi sehemu ya ngozi iliyoathirika huchukuliwa kwa ajili ya kufanya vipimo vya maabara na kuangalia aina sahihi ya fangasi na pale inapothibitika matibabu huanza.
Mara nyingi mapunye hutibika kwa dawa za kutibu fangasi za kupaka ambazo hutibu mapunye na kuyaponyesha kabisa bila kuhitaji kutumia dawa za kumeza. Hii ni kwa kuwa ni rahisi kwa dawa ya kupaka kupenya kwenye ngozi na kusababisha matokeo yanayohitajika. Matibabu ya mapunye huchukua muda mfupi lakini huonyesha matokeo mazuri na kwa bahati matibabu ya fangasi huleta matokeo chanya mara zote. Lakini huwa ni rahisi kwa maradhi hayo kurudi baada ya kumaliza matibabu kama hatua madhubuti za kujikinga na maradhi haya hazitochukuliwa. Kwa sababu hiyo, ni vizuri kwa mgonjwa wa fangasi kutumia dawa mpaka wiki mbili baada ya dalili za maradhi kutoweka. Lakini je ni vipi tunaweza kujikinga tusipatwe na ugonjwa wa mapunje?
Wapenzi wasikilizaji kama tulivyosema magonjwa mengi ya fangasi hujirudia kwa waathirika hata baada ya matibabu iwapo hawatozingatia njia sahihi za kujikinga na maradhi hayo. Kuna mbinu mbalimbali za kujilinda usipatwe na mapunye na fangasi kwa ujumla. Kwanza kabisa ni kuhakikisha kwamba mwili wako hasa kichwani muda wote ni mkavu. Hii ni kwa sababu kama tulivyosema faghasi hupenda kumea katika sehemu nyevunyevu. Pia hakikisha kwamba unaosha nguo, taulo na mashuka mara kwa mara ili kuhakikisha kwamba fangasi wanaondolewa na pia epuka kushirikiana vifaa vya kunyolea nywele hasa kama hakuna namna ya kuvisafisha na dawa maalumu ya kuua vimelea kabla hujatumia kifaa hicho. Njia nyingine ya kujikinga na maambukizi ya fangazi ni kuepuka kushirikiana katika utumiaji wa vifaa vya kufanya usafi wa mwili kama mataulo. Pia kama kazi yako inahusisha ukaaji wa muda mrefu kwenye maji basi hakikisha kwamba unakausha mwili hasa sehemu za kichwa au unaweka dawa ya kuzuia fangasi kwenye maji hayo unayotumia.
&&&&&&&&&&&&&&
Na tunahitimisha kipindi chetu cha leo kwa kuelezea faida za papai. Tunda hili lenye ladha nzuri kama sukari, siyo tu ni tamu kulila, bali pia ni chanzo kikuu cha virutubisho muhimu vinavyotoa kinga ya mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali, na kuukinga na maradhi tofauti. Inaelezwa kuwa papai ni kinga ya ugonjwa wa moyo unaotokana na kuziba kwa mishipa ya damu na ule unaotokana na kupatwa na kisukari. Tunaelezwa kuwa kwa kula papai mara kwa mara tunaweza kuepusha magonjwa hayo yanayosababisha kifo haraka. Pia papai limeonesha kuwa na uwezo mkubwa sana wa kutoa kinga dhidi ya ugonjwa wa saratani ya utumbo ambayo hutokana na mtu kuwa na matatizo katika mfumo wake wa usagaji chakula. Kwani tunda hilo huboresha mfumo mzima wa usagaji chakula na kumfanya mtu kupata choo laini na hivyo kujiepusha na madhara ya kukosa choo kwa muda mrefu ambayo humuweka katika hatari ya kupatwa na kansa ya tumbo. Watu wanaosumbuliwa na majipu au kutokwa na vimbe za ajabu ajabu pamoja na vidonda mara kwa mara, sababu kuu mara nyingi huwa ukosefu wa virutubisho muhimu vinavyopatikana kwenye tunda hili. Imegundulika kuwa, watu wenye matatizo hayo wanapotumia papai au virutubisho vyake, hupata nafuu haraka na kupona matatizo hayo. Vitamin C na Vitamin A ambayo inapatikana mwilini kutokana na kirutubisho aina ya beta-carotene kilichomo kwenye papai, ni muhimu sana kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili dhidi ya magonjwa yanayojirudia mara kwa mara kama vile mafua, maambukizi ya sikio, kikohozi na kadhalika. Pia papai huongeza nuru ya macho kama zinavyoaminika karoti katika suala hilo. Wataalamu wa lishe wanasema kuwa, watu wanaotumia tunda hili hujipa kinga madhubuti ya macho na pia kudhibiti kasi ya kuzeeka ambayo hutokana na kuongezeka umri.
Vilevile kama wewe ni mvutaji sigara au mtu ambaye katika mazingira yako unayoishi unakumbana na moshi wa sigara, basi utumiaji wa vyakula vyenye kiwango kikubwa cha vitamin A kama papai, hukuepusha kupatwa na madhara yanayotokana na moshi wa sigara. Ulaji wa papai pia huepusha hatari ya kupatwa na ugonjwa wa saratani ya kibofu cha mkojo. Suala hilo limeeelezwa katika utafiti wa hivi karibuni uliochapishwa na Asia Pacific Journal of Clinical Nutrition. Kwa ajili hiyo wapenzi wasikilizwaji tujitahidi kula tunda la papai ili kupata faida hizi na nyinginezo, na kujiepusha na magonjwa hatari yanayosumbua watu kila siku.