Meneja mpya wa kikosi cha Simba Mussa Hassan Mgosi ameweka wazi vitu atakavyoanza kuvifanyia kazi ndani ya klabu hiyo ambayo ameitumikia kwa vipindi viwili tofauti kabl ya kuamua kustaafu mwishoni mwa juma lililopita.
Mgosi ambaye alitimkia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika klabu ya Daren Motema Pembe na badae kurejea tena nchini na kuitumikia JKT Ruvu kabla ya kwenda Mtibwa Sugar na hatimae kurejea Msimbazi, amesema dhamira yake kubwa ni kuhakikisha heshima wa Simba inarejea kwa kuwahamasisha wachezaji waliosajiliwa kwa ajili ya msimu wa 2016/17.
Amesema kiu yake kubwa ni kutaka kuona heshima na mafanikio ya Simba yanarudi kama ilivyokua miaka ya nyuma kabl ya kuanza kusota katika nafasi ya tatu hadi ya nne katika msimamo wa ligi kuu tangu mwaka 2011.
“Kazi yangu kubwa sasa ni kuwahimiza wachezaji wajue Simba inahitaji nini na ukiwa Simba unatakiwa ufanye nini,” amesema Mgosi, akitaja baadhi ya mambo ambayo ataanza kufanyia kazi akiwa kama manager mpya wa ‘Wekundu wa Msimbazi.’
“Kipindi cha nyuma wachezaji wa Simba walikuwa wanajua majukumu yao, walicheza kwa kuitumikia timu na walikuwa hawakubali kushindwa pia kulikuwa na ushindani kwasababu kila mmoja alikuwa anataka kucheza na kutengeneza nafasi yake kwenye timu.”
“Navikumbuka sana hivyo vitu ndiyomaana kazi kubwa tangu msimu uliopita ni kuwahimiza wachezaji ili kuendana na ile Simba ya kipindi cha nyuma ambapo kila mchezaji alipambana kuipigania timu kwasababu hakukua na mtu aliyekuwa akikubali kushindwa.”