SERIKALI imetangaza kununua rada mbili mpya kwa ajili ya kusaidia kukusanya mapato, zaidi ya Sh bilioni 18 ambazo zinapotea kila mwaka kutokana na kukosekana udhibiti katika anga la Tanzania.
Kauli hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Ujenzi na Teknolojia, Edwin Ngonyani, kwenye mkutano uliowakutanisha wataalamu wa masuala ya anga pamoja na wamiliki wa kampuni za ndege barani Afrika.
Alisema katika awamu ya kwanza, Serikali imetenga bajeti kwa ajili ya kununua rada mbili ambazo zitafungwa kwenye viwanja vya ndege vya Mwalimu Julius Nyerere na Kilimanjaro (KIA), huku awamu ya pili ikifungwa katika viwanja vya Mwanza na Songwe.
“Serikali tayari imeshatenga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha kuwa inanunua rada mbili, ili kuokoa kiasi cha takribani bilioni 18/- ambazo zimekuwa zikipotea kila mwaka, jambo ambalo linafanya nchi kupoteza mapato, kwani inakuwa haiwezi kulisimamia anga lake lote na hivyo kufanya ndege, hata zile zisizotua nchini huku zikitumia anga hilo, kushindwa kulipa ushuru.
“Kwa sasa Kenya na Rwanda ndiyo nchi zenye rada hizo licha ya kuwa nchi hizo ni ndogo ukilinganisha na Tanzania, rada hizi kila moja inauzwa dola za Marekani milioni 24. Unapoagiza unatakiwa kulipia nusu ya gharama na pindi inapokamilika unamalizia nusu iliyobaki,” alisema Naibu Waziri Ngonyani.
Kwa upande wake, Mkurungezi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TCAA), Hamza Johari, alisema kuwa ununuzi wa rada hizo utasaidia kuongeza mapato na hivyo kufanya viwanja vya ndege kujiendesha vyenyewe bila kusubiri msaada kutoka serikalini.
Katika hatua nyingine, Johari alisema kuwa mamlaka hiyo imesema Tanzania bado haijafikia kiwango cha utengenezaji ndege na hivyo kuwapiga marufuku wanaofikiria kuzitengeneza bila kuwa na kibali cha mamlaka hiyo.
“Ili kuunda ndege unatakiwa kuwa na zana za kisasa… Kwa Tanzania bado hatujafikia uwezo huo, hivyo kama TCAA tunatoa wito kwa wale wote wanaotaka kufanya hivyo bila kushirikisha mamlaka, kuacha mara koja mpango huo kwani ndege hizo wanazotengeneza bila kufuata taratibu, ni hatari na zinaweza zisimudu kukaa hewani muda mrefu na hivyo kusababisha hatari kubwa.
“Hivyo kama mtu anafikiri kuwa ana mawazo ya kutaka kutengeneza ndege, ni lazima aanzie kwetu ili tumshauri kupitia wataalamu wetu na si vinginevyo,”alisema Johari.
Mkutano huo ulikuwa ukikutanisha wamiliki wa ndege zilizokidhi vigezo na wadau mbalimbali wa masuala ya anga kutoka kote Afrika, ukiwa na lengo la kujadili changamoto zilizopo kwenye sekta hiyo.