Wakati akizungumza na Maafisa wa Jeshi la polisi aliowapandisha vyeo vya Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema kipindi cha nyuma jeshi la polisi lilikuwa linaweka historia mbaya.
Kuna baadhi ya polisi waliowahi kuumizwa siku za nyuma kutokana na kusimamia sheria. Kuna magari au mabasi ya wakubwa ndani ya polisi ambayo ilikuwa ukiyakamata unapata msukosuko kikazi na kimaisha.
Rais akatolea mfano akisema kulikuwa na mabasi yanayoitwa Buffalo, Happy Nation au Happy Tanzania ambayo ukiyagusa lazima utaondolewa kwenye cheo ulichopo.
Rais akawaomba Makamishna kwenda kufanya kazi bila woga na wahakikishe pia hawawabughudhi Maaskari walio chini yao wakati wanatimiza majukumu yao ndani ya sheria na Kanuni za utumishi wao.
‘’Hata kama askari atakamata gari la IGP, RPC, Waziri au Rais, mwacheni atimize majukumu yake ili wahusika wa hayo magari wakajieleze wenyewe mbele ya sheria. Sheria ni msumeno’’. Rais alisema.
Rais aliendelea kusema, ‘’tunawanyima nguvu hawa Maaskari wa chini wanapotimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria halafu tunawaambia liachie hilo gari. Akishatoka pale yule aliyekuwa amekamatwa huanza kutamba kweli kweli huku askari akiwa amevunjika moyo na nguvu katika kusimamia sheria. Niwaombe sana, Vyeo vyetu tuweke pembeni na sheria tuziweke pembeni’’.