Askari watano wa Jeshi la Polisi jana waliuawa kwa kudunguliwa na mtu asiyejulikana mitaa ya Dallas nchini Marekani, wakati wa maandamano makubwa ya kupinga mauaji ya watu wawili weusi yaliyofanywa na askari wa kizungu wiki hii.
Ripoti ya jeshi la polisi limeeleza kuwa mbali na askari hao waliouawa, askari wengine wanne wa jeshi la polisi na afisa mmoja wa usafiri wa mwendo kasi walijeruhiwa vibaya.
Mkuu wa Jeshi la Polisi wa Dallas, David Brown aliwaambia waandishi wa habari kuwa maafisa wa Polisi walikuwa katika hatua za kumtia nguvuni mtuhumiwa mmoja kutokana na tukio hilo, na kwamba wakati wanajaribu kuzungumza naye akiwa mbali akiwa ameshikilia bunduki alieleza kuwa alikuwa amekasirishwa na vitendo vya mauaji ya polisi wazungu dhidi ya weusi yaliyofanyika Alhamisi.
“Alisema alitaka kuwaua wazungu,” Brown alieleza.
Baada ya majibizano ya risasi na mtu huyo aliyetajwa kwa jina la Micah Xavier Johnson, polisi walituma robot lenye vilipuzi ambavyo vilimuua.