Mvutano wa kisiasa baina ya vijana wa CCM na CHADEMA kuhusu katazo la mikutano ya vyama vya siasa umezidi kukua huku jeshi la polisi likitarajiwa kutoa tamko kuhusu hali hiyo.
Hali hiyo ya jino kwa jino imejitokeza zikiwa zimebakia siku 16 kabla ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa CCM July 23, ambao Baraza la Vijana la CHADEMA ( BAVICHA ) limesema litawasaidia polisi kuuzuia.
Tayari BAVICHA limetangaza kuandaa vijana 5000 kutoka sehemu mbalimbali nchini kwenda kuzuia mkutano huo utakaotumika kumkabidhi Rais John Magufuli uenyekiti wa chama hicho.
Jumatatu iliyopita, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka aliionya Bavicha wasiende Dodoma kuzuia mkutano wa CCM kwa kuwa watatumia kila mbinu kuwazuia ili kulinda heshima ya chama chao.
Shaka alisema mkutano huo utafanyika kama ulivyopangwa, hivyo Bavicha kama kweli ni vidume wa mbegu wajitokeze ili wakione cha mtema kuni.
Shaka alisema UVCCM wako tayari kuidhihirishia dunia kwa kuwatia adabu Bavicha na kuonya wasijaribu kufanya jambo lolote linalotishia kuhatarisha usalama au ustawi wa maendeleo ya kisiasa ya CCM kwa saa, siku, wakati na mahali popote.
Shaka aliwataka Bavicha kuacha siasa za mikwara, vitisho, kutishia usalama na amani ya nchi kwa kujifanya vijogoo wakati hawana lolote wanaloweza ama kuzuia, kujenga au kubomoa.
Alipoulizwa kuhusu mvutano huo, Msemaji wa Polisi nchini, Advera Bulimba alisema jeshi hilo litatoa taarifa na ufafanuzi kuhusu zuio la mikusanyiko ya vyama vya siasa leo.
Sintofahamu ilivyoanza
Utata huo uliibuliwa na amri ya Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi Makao, Nsato Mssanzya ya kuzuia mikutano na maandamano yote ya vyama kwa madai kwamba vyanzo vyake vya kiintelejensia vilibaini kuwapo kwa uwezekano wa kutokea kwa vurugu.
“Jeshi la polisi nchini linapiga marufuku maandamano na mikutano yote ya hadhara kuanzia Juni 7, mwaka huu hadi hapo hali ya usalama itakapotengamaa."Ilisema sehemu ya taarifa ya jeshi la polisi
Baada ya katazo hilo, jeshi hilo lilitawanya mikutano ya ndani ya Chadema, yakiwamo mahafali ya vijana wa chama hicho (Chaso) yaliyopangwa kufanyika Dodoma kwa madai ya kuwapo mlipuko wa ugonjwa usiofahamika.
Hatua hiyo ya polisi ilikuja baada ya Chadema kutangaza mpango wa kuzunguka nzima kueleza masaibu ya kidemokrasia yanayokikumba na baadaye CCM kutangaza kupita katika maeneo hayo ‘kufuta nyayo”.
Katibu wa Bavicha, Julius Mwita alisema mpaka jana tayari vijana 5,000 walikuwa wakijiandaa kwenda Dodoma; “kushirikiana na polisi kuwafundisha CCM kuheshimu amri zinazotolewa na viongozi. "
"Tumeandaa vijana 5,000 kutoka mikoa 19 nchini ambao wamejitolea kwa nauli zao kwenda Dodoma kushirikiana na jeshi la polisi kuhakikisha mkutano wa CCM haufanyiki.”
Watembelea Butiama
Katika hatua nyingine, viongozi wa Chadema juzi walitembelea kaburi la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere huko Butiama, wakisema walikwenda kumshtaki Rais Magufuli kwa kuminya demokrasia.
Mwenyekiti wa Bavicha, Pastrobas Katambi alisema chama hicho kinatambua jitihada zilizofanywa na Mwalimu Nyerere katika kukuza na kuendeleza ustawi wa jamii ya kidemokrasia nchini.
“Tunapenda kuwaambia watawala kwamba amani ni tunda la haki na ni muhimu utawala ukaheshimu misingi ya kikatiba iliyoachwa na Baba wa Taifa,”alisema Katambi.
Kauli za CCM, Chadema
Naibu Katibu Mkuu Chadema, John Mnyika alisema anabariki maandalizi ya mpango na kitendo kinachotarajiwa kufanywa na Bavicha ili kuwepo na usawa wa kidemokrasia.
“Kama ni ruhusa iwe kwa wote na kama zuio liwe kwa wote, haina maana Chadema wazuiwe lakini CCM waendelee na mikutano yao ya kisiasa,” alisema Mnyika.
Kaimu Katibu wa CCM, Mkoa wa Dodoma alisema mkutano huo ni wa kitaifa na wala si wa mkoa na kushauri atafutwe Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka.
“Sisi tunatekeleza maagizo tunayopewa na si vinginevyo,” alisema. Ole Sendeka hakupatikana na simu yake ilikuwa inaita bila kupokelewa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema mkutano wa CCM ni wa ndani wala hakuna tatizo lolote kwa kuwa mikutano ya ndani inaruhusiwa na kuwa jeshi hilo litawalinda wanaCCM.
Kuhusu Jeshi hilo kuzuia mikutano ya Chadema, Mambosasa alisema walizuia bendera na si vinginevyo na kuwa alitoa taarifa ikiwa kamili lakini waandishi walipotosha.
Manyara wajiandaa
Zaidi ya vijana 560 wa Mkoa wa Manyara, wamejiandikisha tayari kuelekea Dodoma kwa ajili ya kuwasaidia polisi kuzuia mkutano wa CCM ili kuunga mkono agizo la kupigwa marufuku mikusanyiko ya kisiasa.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Francis Massawe aliwataka vijana hao kuachana na mpango huo wa kitoto kwani wao wamejipanga kushughulika na watu wanaotaka kuanzisha vurugu.
Kamanda Massawe alisema endapo kuna kundi linataka kukwamisha mkutano halali wa CCM wa kumchagua mwenyekiti wao, wasubiri hadi mwaka 2020 ndipo wafanye na kwamba polisi hawatakubali hilo litokee.
“Hao vijana wanacheza ngoma ya kitoto ambayo haikeshi kwani wanaingilia majukumu ambayo siyo yao, uchaguzi wa CCM hauna ubishi lazima ufanyike na hakuna wa kuzuia, hao wanacheza kombolela,” alisema.
Msimamo wa Zitto
Akizungumzia uamuzi wa Bavicha, Kiongozi wa ACT Wazalendo ambacho pia mitano yake imezuiwa, Zitto Kabwe alisema haoni tatizo kuhusu suala hilo kwa kuwa wanafanya siasa, hivyo haoni kama ni njia mbaya.
Zitto alisema chama chake hakiwezi kusema moja kwa moja kuwa kinaunga mkono uamuzi wa Bavicha lakini wao watakwenda mahakamani kupinga hatua ya Serikali kuzuia uhuru wa vyama vya siasa kufanya mikutano yao.