Na Baraka Mbolembole
WAKATI vinara wa kundi A katika Caf Confederation Cup 2016, timu ya TP Mazembe ya DR Congo ikijiandaa kwa game yake ya tatu na ya pili ugenini dhidi ya MO Bejaia ya Algeria, wawakilishi wa Tanzania, Yanga SC kwa namna yoyote watapaswa kupata ushindi wa kwanza katika kundi watakapowakabili Medeama ya Ghana katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam siku ya Jumamosi hii.
Yanga wanaburuza mkia katika kundi wakiwa hawana pointi yoyote kufuatia kuchapwa 1-0 na Bejaia (ugenini katika mchezo wa kwanza) kisha 1-0 nyumbani dhidi ya Mazembe. Medeama walipoteza 3-1 katika mchezo wao wa kwanza walipocheza ugenini dhidi ya Mazembe, wakalazimishwa suluhu (0-0 nyumbani) na MO Bejaia.
Kwa maana hiyo angalau wao kuliko Yanga hadi sasa katika michuano kwa maana wamefanikiwa kufunga walau goli moja na kupata alama moja katika game zao mbili za awali.
Kwa sasa hii inachukuliwa kama game inayowakutanisha vibonde wa kundi lakini katika ‘Jicho langu la 3’ naona ni mechi muhimu sana kwa kila timu na hata Mazembe na MO Bejaia watakuwa wakitega sikio zao kujua nini kitakachotokea.
Kama Yanga watachanga karata zao vyema na wakapata ‘funguo za magoli’ ushindi unaweza kuwasogeza katika hatua ya nusu fainali.
Pointi 3 ni muhimu sana kwa kikosi cha Hans Van der Pluijm na Mholland huyo ameshasema wana kila sababu ya kushinda ila si jukumu lake pekee kufanikisha bali ni kazi ya uhakika itakayofanywa na wachezaji wake ndani ya uwanja.
Donald Ngoma hapana shaka ni kipenzi cha mashabiki wa kandanda nchini si wale wa timu yake ya Yanga pekee lakini ‘tabia mbaya anayodaiwa kumuonesha’ mshambulizi mwenzake Amis Tambwe wala si ya kujivunia.
Inasemekana wawili hao (Ngoma na Tambwe) walitofautiana wakati timu hiyo ikiwa katika kambi nchini Uturuki. Sababu kubwa ni Ngoma kumwambia Tambwe kwamba ‘nyakati zake za kutamba klabuni hapo zimekwisha’ kutokana na ujio wa mshambulizi, Mzambia, Obren Chirwa aliyejiunga na Yanga wakati huu wa usajili akitokea FC Platnum ya Zimbabwe.
Hakuna ubishi kwamba Tambwe ni mfungaji namba moja katika timu hiyo. Takwimu zake zinajieleza lakini Ngoma ni kama ana mtafutia nafasi kinguvu rafiki yake Chirwa. Anachopaswa kufanya katika game ya Jumamosi hii ni kutoa ushirikiano wa kila namna kwa Tambwe na amuache Chirwa aingie kikosini kwa uwezo wake.
Yanga haitafunga kwa mara nyingine ikiwa Ngoma ataendelea kumbania Tambwe lakini wakipeana ushirikiano sina shaka Yanga wataanza kushangilia magoli katika michuano hii baada ya kucheza kwa zaidi ya dakika 180 bila kutikisa nyavu za wapinzani wao.
Safu ya ulinzi imeruhusu magoli mawili katika game mbili zilizopita. Si wastani mbaya ukizingatia ni timu moja tu haijaruhusu nyavu zake hadi sasa katika kundi A (Bejaia.) Game moja waliyokwisha cheza ugenini, Medeama waliruhusu magoli matatu.
Kwanini Yanga wasifunge dhidi ya timu hii ambayo ni sawa na ‘Ngazi ya Plastic’ unayoweza kuitumia hata katika nguzo zenye umeme? Tambwe, Ngoma, Chirwa watakuwa na sababu gani ya kusajiliwa kama wataendelea kushindwa kufunga hata dhidi ya timu hii isiyo na uzoefu?
Nidhamu nzuri ya kujilinda katika game dhidi ya MO Bejaia na Mazembe itawasaidia zaidi kama itaendelezwa dhidi ya waghana hawa ambao pia wanasaka alama 3 za kwanza.
Baada ya mechi tutazungumzia mwelekeo wa mabingwa wa Tanzania Bara, lakini bila ushindi ni sawa na kushindwa mapema kusonga mbele. Medeama ni sawa na ‘ngazi ya plastic’ itakayotumiwa na Yanga SC kusonga nusu fainali CAF. Kuna pointi 6 hapa… .Kila la heri Yanga SC.
Kwa ukaribu zaidi, tafadhali unaweza ku-LIKE PAGE yangu BSports. Utapata Updates za michuano mbalimbali.