SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 1 Juni 2016

T media news

VODACOM GLOBAL WAWASOGEZA WASANII KWA MASHABIKI WAO

Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu akiongea na wanahabari wakati wa uzinduzi huo leo.

KAMPUNI ya Vodacom Tanzania kwa kushirikiana na Global Publishers & General Enterprises Ltd, leo wamezindua huduma itakayowawezesha wateja wake kupata habari juu ya maisha ya kila siku ya wasaniii mbalimbali hapa nchini.Akizungumza na wanahabari katika makao makuu ya Vodacom yaliyopo Mlimani City jijini Dar es Salaam, Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu, alisema huduma hiyo itagharimu kiasi cha shilingi mia moja tu (100/=) kwa siku, ambapo mteja atakuwa akipokea taarifa za msanii aliyemchagua kila siku kwa bei hiyo.

“Ili kujiunga na huduma hii, mteja anatakiwa kutuma jina la msanii mfano, Shilole au Kajala kwenda namba 15542, na hapo moja kwa moja atakuwa amejiunga na kuanza kupata habari za msanii husika.

“Kila siku mteja atakuwa anakatwa Sh 100 kwa ajili ya huduma hiyo, pia kwa kiwango hicho cha fedha kwa siku moja anaweza kupata taarifa za msanii huyo kadiri zitakavyokuwa,” alisema Nkurlu.

Aidha, alifafanua kuwa huduma hiyo inalenga kuwaunganisha wateja wa Vodacom na wasanii wao pendwa ili kuwaweka karibu, hiyo ikiwa ni jitihada zao kabambe za kutumia teknolojia kurahisisha na kufanya maisha kuwa murua.Aliongeza kuwa japokuwa huduma hiyo imeunganishwa moja kwa moja, lakini mteja bado anao uwezo wa kujiondoa wakati wowote.Naye Meneja Mkuu wa Kampuni ya Global Publishers, Abdallah Mrisho, alisema hatua hiyo ni nzuri kwani kutokana na jinsi teknolojia inavyokua, hawana budi kuwakutanisha wasanii na mashabiki wao kwa njia yoyote ile lengo likiwa ni kuongeza ukaribu wao.

Katika hatua nyingine, Mrisho aliwataja baadhi ya wasanii ambao tayari wameshaingia kwenye mfumo huo kuwa ni Kajala Masanja, Wema Sepetu, Aunty Ezekiel, Jacqueline Wolper, Shilole na Rose Ndauka na kuongeza kuwa wapo kwenye mazungumzo na wasanii wengine na wana imani wasanii hao wataongezeka.

NA DENIS MTIMA/GPL