SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 2 Juni 2016

T media news

RAIS WA ZANZIBAR DK. ALI MOHAMED SHEIN ATOA PONGEZO KWA SERIKALI JAMHURI YA WATU WA CHINA


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Ali Mohamed Shein akizungumza na Ujumbe wa Chama cha Kikoministi cha China kutoka Kamati ya Jimbo la Jiangsu ukiongozwa na Katibu wake  Bw.Luo Zhijon,(wa tatu kulia) mara  ujumbe huo ulipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo

jioni,[Picha na Ikulu.] 02/06/2016.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa pongezi kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya afya.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika mazungumzo kati yake na Katibu wa Chama cha Kikomunisti cha China katika Kamati ya Jimbo la Jiangsu Bwana Luo Zhijun akiwa amefuatana na ujumbe wake uliofika Ikulu mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alisema kuwa azma ya Jimbo la Jiangsu kuendeleza mashirikiano yake kwa kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo nchini ni hatua moja wapo ya kukuza uhusiano wa kidugu uliopo kati ya pande mbili hizo.

Dk. Shein alipongeza azma ya Kiongozi huyo katika kuimarisha uhusiano katika sekta ya afya, elimu, viwanda, uekezaji, utalii pamoja uvuvi kati ya Zanzibar na Jimbo hilo la Jiangsu.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar itaweza kufaidika kwa kiasi kikubwa na makubaliano ya awali juu ya mafunzo kwa madaktari na wauguzi wazalendo kati yake na Jimbo hilo, kwani ni hatua kubwa katika kuhakikisha sekta ya afya inaimarika hapa nchini.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi na shukurani kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kupitia Jimbo la Jiangsu kwa  utamaduni wa kuendelea kuwaleta Madaktari bingwa kutoka Jimbo hilo tokea mwaka 1964, ambapo mbali ya wataalamu hao pia, nchi hiyo imeweza kuleta wataalamu wake mbali mbali  hapa Zanzibar.

Aidha, Dk. Shein alitoa shukurani kwa chama cha Kikomunisti cha China kwa kuendeleza ushirikiano wake na chama tawala cha CCM na kuahidi kuendeleza mashirikiano hayo kwa kupanua wigo katika nyanja mbali mbali za maendeleo.