Wakati Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza likiwashikilia watu 14 kwa tuhuma za mauaji ya watu watatu katika Msikiti wa Rahman uliopo Ibanda, Kata ya Mkolani mjini Mwanza, Mkuu wa mkoa huo, John Mongella amesema mauaji hayo hayana sura ya ugaidi.
Mongella amesema mauaji hayo hayafanani na vitendo vya aina hiyo, hivyo ni vigumu kuyahusisha na ugaidi bali ni uhalifu kama ulivyo mwingine.
Bila kufafanua, alisema mauaji mengine yanasababishwa na ndugu na jamaa za marehemu. Kadhalika, aliwataka viongozi wa mtaa huo kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi vitakavyoweza kukabiliana na uhalifu wa aina hiyo.
Mauaji hayo yalitokea Mei 18, saa mbili usiku wakati waumini hao wakiwa msikitini wanaswali.
Waliouawa katika tukio hilo ni Imamu wa msikiti huo, Feruz Ismail, Mbwana Rajabu na Khamis Mponda, wakazi wa Ibanda na kumjeruhi Ismail Ghati.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika msako dhid ya wahalifu unaoendelea maeneo mbalimbali mkoani humo.
Hata hivyo, alisema bado hawajamkamata mtuhumiwa aliyempiga risasi Mwenyekiti wa Mtaa wa Bulale, Kata ya Buhongwa jirani na ya Mkolani.
Mwenyekiti huyo Alphonce Nyinzi (48), alipigwa risasi Mei 22, saa moja usiku muda mfupi baada ya kumaliza kuongoza kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mtaa huo.
Kamanda Msangi aliwataka wananchi kutoa ushirikiano ili kuwabaini watu wanaoendeleza uhalifu katika mkoa huo.
“Nawaomba wananchi watupatie ushirikiano maana sisi wenyewe hatuwezi kufanya kazi bila ya kupata ushirikiano wao kwa sababu jamii yenyewe ndiyo inayoishi na watu hao, tuleteeni taarifa za uhalifu tutazifanyia kazi,” alisema.
Kwa kipindi cha wiki mbili mkoani Mwanza, watu 12 wameuawa kwa kukatwa mapanga na shoka, mmoja kwa kupigwa risasi na watu wasiofahamika.