SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 18 Aprili 2016

T media news

SIPENDI SIMBA IWE KAIZER CHIEFS, HANS POPPE AWE KAIZER MOTAUNG MRADI WA BOKO

Na Athumani Adam

Nadhani unaifahamu Kaizer Chiefs, klabu ya mpira wa miguu yenye makazi yake jijini Johannesburg maeneo ya Soweto. Inasemekana ni klabu yenye mafanikio zaidi nchini Afrika Kusini, wana vikombe vya ndani takribani themanini tangu ilipoanzishwa mwaka 1970 na aliyekuwa mchezaji wa zamani wa Orlando Pairets, wapinzani wa Kaizer Chiefs Bw Kaizer Motaung.

Kaizer Motaung aliporudi kutoka Marekani alipokuwa anacheza soka la kulipwa aliamua kuanzisha klabu ikaitwa Kaizer Chiefs maarufu kama ‘Amakhosi’. Licha ya mafanikio ya Kaizer Chiefs timu ya mchezaji wa zamani ya Leeds United ya Uingereza Lucas Radebe, lakini wamezunguka viwanja vipatavyo tisa kuchezea mashindano mbalimbali kama viwanja vyao vya nyumbani.

Mwaka 2006 walianza kujenga uwanja wao wa nyumbani, uwanja ambao ungeitwa jina lao la utani yaani Amakhosi Stadium. Bajeti ya takribani rand bilioni 1.2 za Afrika Kusini ilikadiliwa kujenga uwanja wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 55,000. Uwanja ambao ungekuwa wa kiasasa ukizungukwa na maduka pamoja na sehemu mbalimbali za burudani pia migahawa. Pata picha tu ya Mlimani city au Quality Centre ziwe ndani ya uwanja wa taifa.

Lakini kutokana na tatizo la fedha, ghafla Kaizer Chiefs pamoja na wabia wengine waliokuwa na nia ya kujenga dimba hili, wakabadili malengo. Bajeti ikabalika kutoka rand bilioni 1.2 za Afrika Kusini hadi kufikia rand milioni 700 pia idadi ya watazamaji ipungue kutoka watu 55,000 na kufikia takribani 30,000 hivi.

Ujenzi ukapangwa kuanza mwaka 2010 na kukamilika 2012. Ilipofika mwezi August 2010, Kaizer Chiefs kupitia kwa bosi wake Kaizer Motaung wakatangaza kujitoa kwenye ubia wa ujenzi wa uwanja wa Amakhosi.

Wakaamua kuendelea kutumia uwanja unaomilikiwa na mamlaka ya viwanja nchini humo. Ule uwanja ambao ulipigwa mchezo wa fainali kombe la dunia 2010 kati ya Uholanzi na Hispania, unajulikana kama FNB Stadium uwanja mkubwa barani Afrika unabeba watu takribani 94,000.

Nimeamua nianze na hadithi ya Kaizer Chiefs kama tahadhari kwa klabu ya Simba ya jijini Dar es salaam. Nimesikia jambo zuri ambalo wekundu hawa wa msimbazi wanataka kufanya, sipendi washindwe kama walivyoshindwa Amakhosi.

Siku mbili zilizopita nilimsikia Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, Mr. Hans Poppe akielezea juu ya kuanza kujenga uwanja wa mazoezi pamoja na hosteli pale eneo lao la Boko jijini Dar es Salaam.

Kwenye mahojiano yake na Sports Xtra ya Clouds Fm siku ya Ijumaa, Hans Pope alisema tayari wameagiza nyasi bandia yaani ‘artificial turf’ pia mradi utagharimu pesa za kitanzania shilingi bilioni 3.

Hans Pope alienda mbele zaidi akasema kutokana na ufinyu wa bajeti wameamua kuanza kidogokidogo huku akisita kumtaja mkandarasi aliyepewa kazi hiyo

Sitaki kuamini kama Hans Poppe anaendeleza zile siasa tulizo zoea kuhusu ujenzi wa viwanja kwa kalabu hizi mbili hapa nchini. Napenda kuona Simba wakifanikiwa kwenye hili ili kuonesha kama inawezekana.

Ushauri wangu kwa Simba ni mmoja tu, wafanye jitihada za hali na mali kumpata mdhamini ambaye atawasaidia kutimiza hili kwa makubaliano maalum. Ikiwezekana wampe haki ya kumiliki hata jina la uwanja yaani ‘Naming Right’ kwani timu nyingi duniani siku hizi wanatumia ujanja huu.

Siku moja niliwahi kumsikia mtaalam mmoja wa uchumi wakati la sakata la Mo Dewji alipotaka kuinunua Simba akisema, Simba inafika thamani ya shilingi bilioni 6 za kitanzania.

Sasa mtashindwa vipi kutimiza mradi wa bilioni 3, wakati asset zako ni bilioni 6? Ni suala na kutumia akili za kichumi tu kufanikisha.

Borussia Dortmund waliwapa kampuni ya bima inayojulikana Signal Insurance Group haki za kumiliki jina la uwanja, ukaitwa Signal Iduna Park badala ya Westfalen Stadium

Man City nao  wakafanya hivyo kwa kampuni ya Etihad uwanja wao ukaitwa Etihad Stadium badala ya ‘City of Manchester’.

Arsenal wakafanya kwa Emirates, Man Utd nao wakabadili uwanja wa mazoezi kama ambavyo Simba wanataka kuujega pale Boko. Wakauita AON training Complex badala ya Carrington.

Simba msikubali kufeli kwenye hili, hatutaki tena iwe siasa bali ni kweli. Hebu kaeni meza moja na NHC, NSSF, PSPF, TIGO, VODACOM, COCA-COLA, AIRTEL, TBL, CRDB, NMB, TCC, NBC na wengine kisha waelezeni hili.

Sitopenda kuona mkiishia njiani kama Kaizer Chiefs walivyoishia kuhusu uwanja wa Amakhosi. Mr Hans Poppe usikubali kuwa Kaizer Motaung mzigo ukufie mikononi mwako.

athumani46664@gmail.com