Tamko hilo limetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servacius Likwelile kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa hivi karibuni Jijini Dar es salaam.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa Washirika wa Maendeleo bado wanaendelea kuisadia Serikali katika bajeti yake na kwamba tuhuma za kujitoa kwa makundi 14 ya kuisaidia bajeti ya Tanzania sio za kweli.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa bado makundi hayo yanaendelea kuisaidia bajeti ya Tanzania ambapo kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Washirika wa Maendeleo nane waliahidi kuendelea kusaidia Bajeti Kuu wakiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika, Canada, Denmark, Umoja wa Ulaya, Finland, Ireland, Sweden, na Benki ya Dunia.
Kwa mwaka wa fedha 2016/2017 baadhi ya Washirika wa Maendeleo wameshathibitisha kusaidia bajeti kuu ya Serikali, Washirika hao ni pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika, Denmark, Umoja wa Ulaya pamoja na Benki ya Dunia.
Washirika wengine wa Maendeleo wataendelea kuisaidia Serikali kupitia wa Mfuko wa Pamoja wa Maendeleo na Miradi.
Washirika hao ni pamoja na Ubelgiji, Canada, China, Denmark, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Hispania, India, Italia, Japan, Korea ya Kusini, Norway, Sweden, Uholanzi, Uingereza, Marekani na Uswisi.
Washirika wengine wa maendeleo ambao wanaisaidia bajeti ya Serikali ni Benki ya Maendeleo ya Afrika, Mashirika ya Umoja wa Mataifa, BADEA, Mfuko wa OPEC pamoja na Saudia Umoja wa Ulaya na Benki ya Dunia.
Taarifa hiyo ya Dkt. Likwelile imeongeza kuwa, Serikali ya pamoja na washirika wa maendeleo wanaoisaidia Tanzania wako katika mazungumzo juu ya namna ya kuimarisha ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Tanzania na nchi hizo.
Serikali imewashukuru Washirika wa Maendeleo kwa kuendelea kuisaidia Tanzania katika kupelekea juhudi za kimaendeleo zenye tija kwa wananchi.