Mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia juzi imeleta athari kubwa katika Kijiji cha Chenene Kata ya Haneti Tarafa ya Itiso, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma na kukosesha makazi zaidi ya kaya 40.
Akizungumza jana, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Farida Mgomi alisema nyumba nyingi zilizobomoka ni zile zilizojengwa kwa matofali ya udongo. Mgomi alisema athari hiyo inaweza kuongezeka kutokana na nyumba kujaa maji na zinaposhindwa kuhimili hudondoka.
“Nyumba nyingi zilijaa maji, kwa hiyo hata chakula, magodoro, nguo vyote vimeharibika,” alisema.
Mgomi alisema tathmini ya awali tayari imefanyika. Na hakuna mtu aliyefariki dunia kufuatia maafa hayo.
“Waathirika wote ambao nyumba zao zimeanguka tayari wamepata sehemu za kujihifadhi kwa msaada mkubwa majirani na kutoka viongozi wa Serikali ngazi ya Kijiji, Kata, Tarafa na Wilaya,” alisema mkuu wa wilaya.
Alisema Kamati ya Maafa ya Wilaya tayari imechukua na inaendelea kuchukua hatua za haraka,kuona namna ya kusaidia familia zilizoathiriwa na maafa hayo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Pia alisema hata baadhi ya mashamba (mazao) yamesombwa na maji.
“Baadhi ya wananchi wamepoteza mali zao hifadhi za chakula katika kaya zao, mabati, vyombo vya ndani na mali nyingine za namna hiyo,”alisema.
Naye Ofisa Tarafa wa Itiso, Remidius Emmanuel alisema mvua hiyo imeacha kaya zikiwa hazina makazi.
“Kaya zaidi ya 40 zimeathirika, nyumba nyingi zilizodondoka ni zile zilizojengwa kwa matofali ya udongo,” alisema Emmanuel na kuongeza kuwa nyumba nyingi zilibomoka kutokana na kujaa maji kutoka milimani.
Pia ujenzi wa barabara ya Kondoa hadi Babati umeonesha kuathiri miundombinu kwani madaraja yaliyojengwa ni madogo yanashindwa kuhimili wingi wa maji kutoka milimani
“Katika eneo la Chenene ujenzi wa barabara unaonekana kuleta athari kwa makazi ya wananchi kwani madaraja ni madogo, maji yanapofika kwenye barabara yanakosa mwelekeo na kurudi kwenye makazi ya watu hali hiyo ikapelekea nyumba kubomoka,” alisema Ofisa Tarafa huyo.
“Nimetembelea maeneo yote yaliyokumbwa na maafa hayo. Nimekutana na kuzungumza na waathirika wote,” aliongeza.