SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 22 Machi 2016

T media news

Watumishi Watatu Manispaa Ya Kinondoni Kusimamishwa Kazi




KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeitaka Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuwasimamisha kazi watumishi watatu wa Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, akiwemo Mwanasheria wa Manispaa hiyo, Barton Mahenge kutokana na matumizi mabaya ya ofisi.

Watumishi wengine waliotakiwa kusimamishwa kazi kutokana na matumizi hayo mabaya ya ofisi na kushindwa kuishauri manispaa hiyo kuhusu mkataba wake na Kampuni ya Oysterbay Villa ni Mchumi Mwandamizi, Ando Mwankuga na Mratibu wa Uwekezaji na Mthamini wa Manispaa hiyo, Einhard Chidaga.

Pamoja na hayo, Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene pamoja na kuahidi kutekeleza maagizo hayo, pia ameapa kuwa atahakikisha watendaji wengine waliohusika katika mkataba huo hata kama wamestaafu au kuacha kazi, wanapatikana na kuwajibishwa.

Akizungumza na uongozi wa manispaa hiyo, Mwenyekiti wa LAAC, Kangi Lugola alisema watumishi hao pamoja na kuwepo kwenye madaraka yao kwa muda mrefu, wameshindwa kushauri namna ya kufikia malengo ya mkataba huo ambayo ni kuongeza mapato na ajira.

Alisema kamati hiyo imebaini kuwa mkataba huo unaohusisha vitalu viwili vilivyopo eneo la Oysterbay namba 277 na 322 vimekuwa vikimnufaisha mwekezaji huyo pekee kwa muda wa miaka sita tangu ujenzi wa majengo ya makazi ukamilike mwaka 2011.

“Kamati hii imetafakari na kuamua kuwa mwanasheria, mchumi na mthamini wa manispaa wasimamishwe kazi ili kupisha uchunguzi dhidi ya mkataba huu. Kamati yangu pia itaunda kamati ndogo itakayoshirikiana na Sekretarieti ya Sheria ya Bunge ili kuupitia kwa kina mkataba huu na kutoa ushauri utakaosaidia manispaa hii,”alisisitiza Lugola.

Alisema baada ya LAAC kupitia mkataba huo imebaini kuwa pamoja na manispaa hiyo kutopata mapato kwa muda wa miaka sita huku majengo yakiwa matupu bila wapangaji kwa kipindi chote, pia uwekezaji wa mradi huo unaojumuisha ardhi, alipatiwa mwekezaji raia wa nje jambo ambalo ni kinyume cha sheria za uwekezaji nchini.

Aidha, alisema mkataba huo umebainisha mgawanyo wa mapato baina ya pande zote mbili zilizoingia ubia ambao hauendani na kiwango cha uwekezaji kwani Manispaa ya Kinondoni iliwekeza kwa kutumia ardhi kupitia vitalu viwili vyenye thamani ya Sh bilioni sita wakati mwekezaji huyo alijenga majengo hayo kwa gharama ya Sh bilioni 11.

“Mkataba unaonesha mgawanyo wa mapato kwa kila upande na upande wa manispaa unapata asilimia 25 kupitia vyumba vyake 17 vya mradi huo, wakati kampuni ya Oysterbay Villa inapata asilimia 75 kupitia vyumba vyake 51,” alisema Lugola katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Naibu Spika Dk Tulia Ackson.

Alisema mkataba huo pia unaonesha kuwa katika kitalu 377 mwekezaji anatakiwa kujenga jengo la ghorofa lenye vyumba 40, lakini katika uhalisia alijenga jengo lenye vyumba 44 huku mgawanyo ukibakia vilevile kama mkataba wa awali ulivyotaka asilimia 25 na 75.

“Hili ndio eneo lenye changa la macho, huu mgawanyo haueleweki na kama kweli mnapata asilimia 25, mbona tangu mwaka 2011 manispaa haijapata hata senti tano ya faida ya mradi huu zaidi ya kudai kuwa mnamdai mwekezaji shilingi bilioni 3.5 tena za miaka hiyo…” 

Pamoja na maagizo hayo, pia kamati hiyo, iliitaka Wizara ya Tamisemi ihakikishe inampatia Mwanasheria Mkuu (AG) wa Serikali mkataba huo ili aupitie na kutoa ushauri wake.