SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 6 Machi 2016

T media news

Upinzani dhidi ya uingiliaji wa kijeshi wa Magharibi nchini Libya

Sanjari na upinzani wa baadhi ya nchi za Kiarabu dhidi ya uingiliaji wa kijeshi wa Magharibi katika mgogoro wa Libya, Waziri wa Afya wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ametoa indhari kuhusiana na kutokea maafa ya kibinadamu katika nchi hiyo.Katika hali ambayo baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kuhusiana na uwepo wa vikosi vya Ufaransa, Marekani, Uingereza na Italia katika ardhi ya Libya, Kanali ya Televisheni ya al-Jazeera ya Qatar imetangaza baada ya kufanya uchunguzi wa maoni kwa watazamaji wake kwamba, asilimia 90 ya watazamaji hao wanapinga nchi za Magharibi kuishambulia kijeshi Libya. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baada ya Marekani kuishambulia kijeshi Afghanistan na Iraq na kuibuka makundi ya kigaidi na kitakfiri katika nchi za Afghanistan, Syria na Iraq wananchi wa nchi za Kiislamu hawana mtazamo mzuri kuhusiana na uingiliaji wa kijeshi wa madola ya Magharibi katika nchi za Mashariki ya Kati.Ramtane Lamamra, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Algeria kwa mara nyingine tena ametahadharisha kuhusiana na uingiliaji tarajiwa wa aina yoyote ile wa kijeshi wa madola ya kigeni nchini Libya na kusisitiza juu ya kutatuliwa kisiasa mgogoro wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Duru za habari zimetangaza kuwa, kikosi maalumu cha Ufaransa, Uingereza, Marekani na Italia kiliingia Libya siku chache zilizopita. Gazeti la Italia la Corriere della Sera limeripoti kwamba, kikosi maalumu cha askari 50 cha nchi hiyo kinaelekea nchini Libya kwa minajili ya kusaidiana na wanajeshi wa Ufaransa, Marekani na Uingereza katika operesheni ya kijeshi dhidi ya kundi la Daesh. Kwa mujibu wa gazeti hilo, operesheni hiyo ya kijeshi ilianza tangu tarehe 10 ya mwezi uliopita wa Februari na kwamba, itaendelea kwa kikosi hicho maalumu kujiunga na vikosi hivyo vya Marekani, Uingereza na Ufaransa. Hayo yanajiri katika hali ambayo, hali ya kibinadamu nchini Libya inaripotiwa kuwa mbaya huku wananchi katika baadhi ya maeneo wakikosa kabisa huduma muhimu. Reida el-Oakley, Waziri wa Afya wa Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya alitangaza siku ya Ijumaa kwamba, hali ya afya katika nchi hiyo ni mbaya na ya kusikitisha mno na akatoa wito wa kuhitimishwa uzuiwaji wa mali za nchi hiyo zilizoko katika nchi nyingine. Amesema, fedha hizo zinaweza kudhamini mahitaji ya dawa ya mwaka mmoja ya wananchi wa nchi hiyo. Baada ya kuangushwa utawala wa Kanali Muammar Gaddafi huko Libya mwezi Oktoba mwaka 2011, vinara wa kundi la kigaidi la Daesh waliainisha nchi hiyo kuwa mahala salama kwa ajili ya kuasisi kambi za kijeshi na kuingia katika nchi nyingine za bara hilo.Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kama hakutachukuliwa hatua za haraka za kuhitimisha mgogoro huo kwa njia za kisiasa, inawezekana nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ikakumbwa na hasara ambazo ufidiaji wake utachukua miaka mingi.