Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen ametangaza kuwa, pande zinazopigana nchini humo zimefikia makubaliano ya kusitisha vita tarehe 10 Aprili.
Ismail. Ould Sheikh Ahmad amewaambia waandishi habari mjini Riyadh kwamba, pande mbili zinazopigana nchini Yemen zimekubaliana kusitisha vita ifikapo Aprili 10 na kuanza mazungumzo tarehe 18 nchini Kuwait. Amesema mazungumzo yajayo yatakuwa fursa ya mwisho kwa ajili ya kukomesha vita nchini Yemen na kuongeza kuwa, pande hizo pia zimefikia makubaliano ya kuunda tume itakayochunguza hali ya watu wanaoshikiliwa nchini Yemen.
Inaonekana kuwa serikali iliyojiuzulu na kukimbia nchi ya Yemen imekubali masharti ya harakati ya Ansarullah na chama cha rais wa zamani wa nchi hiyo Ali Abdullah Saleh kwa ajili ya amani na kuingia kwenye mazungumzo mapya ya kisiasa. Kwani ripoti za duru za Yemen zinasema harakati ya Ansarullah na chama cha Abdullah Saleh vilikuwa vimetoa takwa la kusitishwa vita kikamilifu na kuondolewa mzingiro wa nchi kavu na anga kama masharti ya kushiriki kwenye mazungumzo yajayo. Duru hizo zimesema kuwa, mjumbe wa Umoja wa Mataifa Ould Sheikh Ahmad aliiambia harakati ya Ansarullah na chama cha Saleh kwamba usitishaji vita utahusu maeneo ya mpakani tu lakini harakati ya Ansarullah imetaka kusitishwa mashambulizi ya Saudi Arabia na washirika wake katika miji na maeneo yote ya Yemen na kufutwa mzingiro wa muungano huo dhidi ya watu wa Yemen.
Wakati huo huo ripoti zinasema kuwa Ali Abdullah Saleh amewataka Wayemeni wafanye maandamano ya kupinga vita vya Saudia dhidi ya Waislamu wa Yemen Jumamosi ijayo kwa mnasaba wa kutimia mwaka mmoja tangu watawala wa kifalme wa Riyadh na washirika wao waanzishe mashambulizi dhidi ya nchi hiyo. Abdullah Saleh ambaye ni mwenyekiti wa chama cha Congresi ya Taifa ya Yemen amesema kuwa, nchi hiyo inakabiliwa na uharibifu mkubwa uliosababishwa na mashambulizi ya mwaka mmoja ya wavamizi wa Kisaudi na kwamba msemaji wa serikali ya Riyadh anasema kuwa mashambulizi dhidi ya nyumba na makazi ya raia yataendelea nchini Yemen hadi pale chama cha Congresi ya Taifa na harakati ya Ansarullah itakaposalimu amri kwa matakwa ya Riyadh. Ali Abdullah Saleh ameongeza kuwa, kamwe Wayemen hawatasalimu amri au kulegeza kamba.
Mkuu wa chama cha Congresi ya Taifa ya Yemen amesema kuwa chama hicho kinaiunga mkono harakati ya wananchi ya Ansarullah katika mapambano yake dhidi ya wavamizi na kwamba rais aliyetoroka nchi na kwenda Saudi Arabia amefanya uhalifu na jinai nyingi akishirikiana na wavamizi na kwa msingi huo hastahiki kuwa kiongozi wa nchi hiyo.
Mwishoni mwa mwezi Machi mwaka jana, Saudi Arabia na washirika wake wa Kiarabu wakisaidiwa na Marekani walianzisha mashambulizi makali ya anga dhidi ya watu wa Yemen kwa kisingizio cha kutaka kumrejesha madarakani rais aliyejiuzulu mwenyewe na kutoroka nje, Abd Rabbuh Mansur Hadi. Hadi sasa mashambulizi hayo yameua maelfu ya raia wa Yemen na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.
Katika upande mwingine Abdulsalam al Hijaf ambaye ni mwanachama mwandamizi wa harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah amezitaka nchi mbalimbali duniani kutazama upya uhusiano wao na Saudi Arabia. Amesema kwa kutilia maanani uhalifu na jinai za kutisha zilizofanywa na Saudia na washirika wake, jamii ya kimataifa inalazimika kutazama upya siasa zake katika kuamiliana na serikali ya Riyadh.
Abdulsalam al Hijaf amesema kuwa, mazungumzo ni miongoni mwa misingi mukuu ya harakati ya Ansarullah lakini Saudia haina azma ya kweli ya kufanya mazungumzo na inafanya jitihada za kutaka kulazimisha mipango na matakwa yake kupitia kwa makundi vibaraka na tegemezi.