SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 18 Machi 2016

T media news

Mulongo atua Mara, achimba mkwara

Mkuu mpya wa Mkoa wa Mara, Magessa Mulongo jana, aliwaweka kitimoto viongozi na wakuu wa taasisi za ulinzi na usalama mkoani kwa kupuuza kero za wananchi, ikiwamo ya mauaji ya watu kwa kukatwa mapanga huku wakiyaita kuwa ni matukio madogo ya kihalifu.

“Yaani watu wanakufa halafu mnakuja hapa na kuyaita matukio madogo ya uhalifu? Sitaki kusikia tena kauli hiyo,” alisema Mulongo.

“Jukumu letu kubwa kama viongozi ni usalama wa wananchi na mali zao katika maeneo yetu ya uongozi. Halafu baadhi ya viongozi wenye dhamana ya ulinzi na usalama mnasema hali siyo shwari kwa sababu kuna matukio madogomadogo ya kiuhalifu. Vifo vya watu ni matukio madogo?”.

Mulongo aliyekuwa akizungumza kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kushika wadhifa huo akitokea Mkoa wa Mwanza, aliziagiza kamati za ulinzi na usalama kuanzia ngazi za vijiji hadi mkoa, kukomesha vitendo vyote uhalifu.

“Kuanzia leo ni marufuku vitendo vya watu kuuawa kwa kukatwa mapanga kusikika mkoani Mara. Kila kiongozi atimize wajibu wake,” aliagiza Mulongo ambaye pia ni mzaliwa wa mkoa huo.

Mkuu huyo wa mkoa aliwaagiza makamanda wa polisi Mara na Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya kusimamia kikamilifu utekelezaji wa agizo hilo.

Mulongo alisema imekuwa ni kawaida wananchi kuhofia maisha yao kutokana na mkoa huo kukithiri kwa vitendo vya uhalifu, hususan mauaji.

“Iwe mwisho kwa Mkoa wa Mara kusifika kwa uhalifu. Kila mhalifu anayeingia Mara lazima anaswe na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.”

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Felix Lyaniva na Meya wa Manispaa ya Musoma, William Gumbo walimweleza mkuu huyo wa mkoa kuwa maeneo yao yanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo upungufu wa madawati, vyumba vya madarasa na mauaji ya watu wanaokatwa mapanga na makundi ya wahalifu wasiojulikana.