SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 11 Machi 2016

T media news

KWA NAFASI WALIYOPO, MASTAA MWADUI FC WANASTAHILI MIKATABA MIPYA?



Baada ya kulazimishwa suluhu-tasa na Majimaji FC katika uwanja wake wa nyumbani (Mwadui Complex) siku ya Jumatano, timu ya Mwadui FC ya Shinyanga imeendelea kusalia katika nafasi ya 6 ya msimamo wa ligi kuu Tanzania bara (VPL.)

MSIMU WA KWANZA VPL

Baada ya kushindwa kupanda VPL msimu wa 2014/15, Mwadui FC chini ya kocha Jamhuri Kiwhelo ‘Julio’ ilijipanga tena katika ligi daraja la kwanza (FDL) na kufanikiwa kupanda VPL kama mabingwa wa FDL mapema mwaka 2015.

Julio ambaye ni kocha wa zamani wa timu ya taifa ya vijana ( U23,) na klabu za Simba SC, Ashanti United, na Coastal Union aliwasaini wachezaji zaidi ya 15 wenye uzoefu kutoka klabu za Mbeya City FC, Yanga SC, Kagera Sugar FC na Mtibwa Sugar FC.

Paul Nonga, Anthony Matogolo walisajiliwa kutoka City, Rashid Mandawa, Malegesi Mwangwa walisajiliwa kutoka Kagera Sugar, David Luhende, Jamal Mnyate, walisajiliwa kutoka Mtibwa, Jerry Tegete, Nizar Khalfan walisajiliwa kama wachezaji huru kutoka klabu ya Yanga.

Pia nahodha wa kikosi hicho,Jabir Aziz Stima alijiunga hapo kama mchezaji huru mara baada ya kumaliza mkataba wake katika timu ya JKT Ruvu, mlinda mlango, Shaaban Kado yeye alitokea Coastal Union kama mchezaji huru.

Hawa ni baadhi tu ya wachezaji ambao tayari wamecheza kwa viwango vya juu katika VPL na walisajiliwa na Julio ili kuungana na wakali waliokuwapo tangu timu ikiwa FDL.

Athumani Idd ‘Chuji’, Malika Ndeule, Said Sued, Julius Mrope, Bakar Kigodeko, nyota hawa baadhi walimsaidia sana Julio kuhakikisha Mwadui inapanda VPL, wote hawa wapo kikosini hadi sasa.

MIAKA MIWILI FDL, KISHA MKATABA WA MIAKA MITATU, JULIO ATASHINDWA?

Julio ana nafasi ya kuwa katika timu hiyo kwa miaka mitano, aliifundisha kwa misimu miwili katika ligi daraja la kwanza (2013/14 na 2014/15,) na baada ya kuipandisha VPL akapewa mkataba wa miaka mitatu zaidi. Ni mkataba mrefu kwa kocha kuwa katika timu kwa miaka mitano, lakini je, Julio atafanikiwa?

Mwadui tayari imefanikiwa kupata ushindi katika michezo 9 kati ya 22 waliyokwisha cheza msimu huu (Toto Africans 1-0 Mwadui, Mwadui 2-0 African Sports, Maji Maji 0-1 Mwadui, Mwadui 2-1 Ruvu JKT,  Mwadui 3-1 JKT Mgambo, Stand United 0-2 Mwadui, Mwadui 2-1 Ndanda, Mwadui 2-1 Kagera Sugar, Mwadui  1-0 Toto Africans, Mwadui 2-1 Coastal Union).

Sare 6  (Coastal Union 0-0 Mwadui, Tanzania Prisons 0-0 Mwadui, Mwadui  2-2 Young Africans,   Mwadui 1-1 Simba, Mwadui  0-0 Tanzania Prisons, Mwadui 0-0 Maji Maji) na wamepoteza michezo 7 hadi sasa (Mwadui 0-1 Azam, Mtibwa Sugar 4-1 Mwadui, Mbeya City 1-0 Mwadui, African Sports 1-0 Mwadui, Azam 1-0 Mwadui, Ruvu JKT  1-0 Mwadui).

Ni timu nne tu ambazo zimemudu kushinda michezo kumi na zaidi hadi kufikia raundi ya 22 ya VPL. Kwa nafasi waliyopo si mbaya kwa timu ambayo ndiyo kwanza imetoka kupanda ligi kuu na Julio yuko katika njia nzuri na vijana wake, kwa maana tayari wamekusanya pointi 33 (poimti 3 nyuma ya Mtibwa Sugar walio nafasi ya 4.

Lakini bado Julio atapaswa kuweka mbinu zake za uchezaji ili mashabiki wafahamu kiwango halisi na aina ya uchezaji wa timu yake. Kuwakusanya wachezaji wazoefu ilikuwa ni sahihi kwa maana timu ilikuwa na ina uwezo wa kuwamiliki, lakini stahili yao ya uchezaji ikoje?

Ni timu inayocheza kwa kujilinda zaidi na kushambulia kwa kushtukiza? Au ni timu inayocheza mchezo wa kupasiana na kumiliki mpira huku wakitengeneza nafasi?

Wakati wa kocha Juma Mwambusi katika timu ya Mbeya City aliweza kuifanya timu hiyo iwavutie wengi kutokana na uchezaji wa kushambulia na kuzuia kwa pamoja, lakini nje ya gemu mbili dhidi ya Yanga SC na Simba SC, kikosi cha Julio bado hakivutii kwa namna kinavyokuwa kikicheza. Julio amekuwa akisisita kuhusu ubora kwanza wa mchezaji kabla ya kupampa nafasi mchezaji katika kikosi cha kwanza.

Kufunga magoli 21 tu katika michezo 22 inaonyesha wazi kuwa timu haishambulii vizuri, kuruhusu magoli 18 ni dalili nyingine kwamba katika ngome pia kuna mapengo mengi.

Timu si imara sana katika kujilinda na si kali katila mashambulizi ila kwa namna walivyopambana dhidi ya Yanga na Simba, kisha gemu mbili walizopoteza mbele ya Azam FC inaonesha nguvu ya wachezaji jinsi ilivyo kubwa. Miaka mitano kama kocha, Julio ana nafasi ya kuitengenezea Mwadui FC falsafa yake ya kiuchezaji na si mchezo wa kubahatisha kama ilivyo sasa.

MASTAA WANASTAHILI MIKATABA MIPYA?

Wachezaji kama Mnyate, Stima, Mwangwa, Mandawa, Nizar, Chuji, Mrope wanaelekea kumaliza mikataba yao katika timu hiyo. Je, wanastahili mikataba mipya klabuni hapo au Julio anapaswa kusajili vijana zaidi baada ya timu kupata uzoefu msimu huu.

Kuwa nafasi ya 6 ya msimamo huku wakiwa na gemu 8 kabla ya kumalizika kwa msimu, Mwadui FC ipo katika nafasi stahili lakini viwango vya mastaa vinastahili kuwapa mikataba mipya kwa ajili ya msimu ujao? ‘Kwa nafasi waliyopo, Mastaa Mwadui FC wanastahili mikataba mipya?’