SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 1 Machi 2016

T media news

Hali nchini Syria baada ya kuanza utekelezwaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano

Tangu kuanza utekelezwaji wa makubaliano ya usitishaji vita kati ya serikali na wapinzani huko Syria Ijumaa iliyopita, mambo mengi yamejitokeza ambayo yanatujengea taswira ya jinsi hali halisi ilivyo katika nchi hiyo na eneo zima la Mashariki ya Kati.Kuanza mchakato wa kujiandikisha watu kwa ajili ya kuwania viti vya ubunge kwenye uchaguzi ujao, kuendelea vyema utekelezwaji wa makubaliano hayo ambayo hayayahusishi makundi ya kigaidi kama vile Daesh na Jab'hat an-Nusra, kufukuzwa makumi ya raia wa Syria kutoka Kuwait, radiamali ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria kwa matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Adel al-Jubeiri, pamoja na mashambulizi ya wapiganaji wa Kikurdi dhidi ya ngome za Daesh ni baadhi tu ya matukio hayo ya Syria tangu kupotea kwa kiasi kikubwa sauti za risasi na mizinga katika nchi hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita.Tume ya uchaguzi ya Syria imetangaza kuwa, kufikia jana Jumatatu takriban watu 3000 walikuwa wamejiandikisha kama wagombea wa viti vya ubunge kwenye uchaguzi ujao unaotarajiwa kufanyika Aprili 13 mwaka huu. Tume hiyo sambamba na kuendelea na shughuli za kuwaandikisha wagombea hadi siku ya Alhamisi ya wiki hii, pia imetangaza kwamba, uchaguzi wa bunge utafanyika tu katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali. Wachambuzi wengi wanasema suala la kujiandikisha wagombea wa viti vya ubunge linaonyesha kuna mwanga wa matumaini unaoanza kuonekana kwa mbali katika mustakabali wa taifa la Syria.Katika upande mwingine, serikali ya Syria imetoa radiamali kali kwa matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia Adel al-Jubeiri ambaye siku ya Jumamosi alisema Rais Bashar al-Asad ni lazima aondoke madarakani ima kwa hiari au kupitia nguvu za kijeshi. Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imeitaka Saudia kukoma kuingilia mambo ya ndani ya Damascus na kumtaja al-Jubeiri kuwa ni kibaraka wa Wazayuni na Marekani. Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imesema matamshi ya al-Jubeiri yanaakisi misimamo ya utawala bandia wa Israel pamoja na Marekani.Kuhusiana na utekelezwaji wa makubaliano ya muda ya usitishwaji vita yaliyoanza alfajiri ya Jumamosi Februari 27, duru mbalimbali za habari zinaripoti kwamba mwenendo wa utekelezwaji ni mzuri licha ya kuweko visa vya hapa na pale vya ukiukwaji wake. Taasisi ya kufuatilia utekelezwaji wa makubaliano hayo siku ya Jumapili iliripoti visa 9 vya kuvunjwa makubaliano hayo ya usitishwaji vita na kati ya hivyo, 7 vilifanywa na upande wa upinzani. Russia ambayo kwa miezi kadhaa imekuwa ikiendesha mashambulizi ya kila kona dhidi ya magaidi wa Daesh huko Syria imesema mwenendo wa makubaliano hayo ni mzuri na hadi kufikia sasa ni wa kuridhisha. Makubaliano ya usitishwaji vita kati ya serikali na upinzani yalifikiwa chini ya upatanishi wa Russia na Marekani na yanatarajiwa kudumu kwa siku 10.Kwa maneno machache tunaweza kusema hali ya Syria baada ya kuanza makubaliano ya usitishwaji vita ni yenye kutia matumaini. Hata hivyo, baadhi ya tawala katika eneo la Mashariki ya Kati kama vile Saudi Arabia na utawala ghasibu wa Israel bado zinaleta chokochoko kujaribu kuvuruga na kurudisha nyuma hatua zilizopigwa na jamii ya kimataifa katika kutatua mgogoro wa Syria.