Wakati waziri wa nchi ofisi ya Rais, Tamisemi na utawala bora George Simbachawene akitoa muda wa uchaguzi wa mameya kukamilika ifikapo machi 25 mwaka huu,Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Simba “Gadafi” amemuomba Waziri huyo kuangalia upya utendaji kazi wa wakurugenzi wa Manispaa za Ilala na Kinondoni, akidai wamevuruga uchaguzi wa meya na naibu wake.
Akizungumza na wanahabari jana, Simba alisema CCM imefikia hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na utendaji kazi wa wakurugenzi hao, ikiwamo kushindwa kutafsiri vyema vifungu vya sheria vilivyosababisha kuondolewa kwa majina ya wajumbe wao kwa madai kuwa hawana sifa za kushiriki uchaguzi huo.
“Wakurugenzi hawakuwa majasiri katika kupambana na vitisho vya wajumbe wa Ukawa na kuwa wakweli. Walishindwa kutoa tafsiri sahihi ya wajumbe halali wanaotakiwa kupiga kura katika uchaguzi wa meya wa jiji,” alilalamika Gadafi.
Kwenye mkutano huo Gadafi alidai kwamba wakurugenzi hao walifanya upotoshaji wa tafsiri sahihi kuhusu uwepo wa wajumbe wa CCM walioonekana kutokuwa wajumbe halali.
“CCM imesikitishwa na upotoshaji uliofanywa na wakurugenzi hao hasa kwa kuwavua uhalali wa kupiga kura baadhi ya wajumbe wetu,” alisemea na kuongeza;
“Wakurugenzi wa Manispaa za Ilala na Kinondoni wamekula matapishi yao, haiwezekani uchaguzi wa awali wawakubali wabunge viti maalum kama wajumbe halafu uchaguzi wa jiji waseme hawastahili kupiga kura.”
Gaddafi alidai kwamba, Ukawa ndio walikuwa wa kwanza kuuvuruga uchaguzi huo kwa kuwa walitumia njia ya vitisho na kuwafanya wakurugenzi wafanye maamuzi kulingana na mashinikizo yao.
Alidai kwamba, licha ya CCM kuonekana kuwa chanzo cha kuvuruga uchaguzi huo lakini chama hicho hakina sababu hata moja ya kufanya hivyo isipokuwa ni utaratibu wanaoshinikiza ufuatwe na kuwa wana mgombea bora na anayekubalika.
“Wajumbe wa Ukawa ndiyo walianza kukiuka taratibu za upigaji kura kwa kupiga picha kura walizopiga na kumuonesha mmoja kati ya viongozi wao.
“Uchaguzi hupigwa kwa siri, iweje Ukawa wawalazimishe wajumbe wao kupiga picha kura walizopiga? Ina maana wanaogopa wajumbe wao wasije wakaipigia kura CCM,”alisema.