SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 21 Machi 2016

T media news

Afisa TRA mbaroni kwa tuhuma za rushwa ya mil. 1.5

Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Dodoma inamshikilia ofisa kodi msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Dodoma, Flavian Chacha kwa makosa ya kuomba na kupokea rushwa ya sh. 1.5 milion kutoka kwa mfanyabiashara wa matofali.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Emma Kuhanga amesema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa na TAKUKURU baada ya mfanyabiashara aliyefahamika kwa jina la Jackson Shirima kwenda kutoa taarifa za kuombwa rushwa na Ofisa huyo.

Kuhangwa amesema kuwa Ofisa huyo aliomba rushwa ya sh. 1.5 milioni kwa mfanyabiashara huyo ili asimchukulie hatua kwa kosa la kusafirisha mzigo wa matofali bila kutoa stakabadhi ya mauzo.

Amesema mtuhumiwa ametenda kosa kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Amesema Machi 18 mwaka huu maofisa wa TRA wakiwa katika shughuli zao za kikazi walilikamata lori aina ya Mitsubishi Fuso lililokuwa likiendeshwa na Joshua Charles likiwa na mzigo wa matofali kutoka kiwandani kwa Shirima, ambapo baada ya kulikagua walibaini kwamba mali hiyo iliuzwa bila kutoa stakabadhi, hivyo walimwamuru dereva wa gari hilo kulipeleka ofisi za TRA kwa hatua zaidi.

Amebainisha kuwa baada ya gari hilo kukamatwa, dereva wa gari hilo alimpigia simu tajiri wake (Shirima) ili alete stakabadhi iliyokuwa inadaiwa na maofisa wa TRA.

Ameongeza kuwa baada ya mazungumzo marefu kati ya Shirima na Ofisa wa TRA (Chacha), ndipo alipomweleza Shirima atoe faini ya sh. 3 milion ambapo baada ya kuomba sana ndipo alipopunguziwa hadi sh 1.5 milioni ndipo alipoomba nafasi ya kwenda kuzitafuta fedha hizo.

Kwa upande wake Jackson Shirima amesema kuwa baada ya kuombwa kiasi hicho cha fedha aliamua kwenda moja kwa moja kwenye ofisi za TAKUKURU mkoa wa Dodoma na kutoa taarifa za tukio hilo ambapo baada ya kujiridhisha kuwa kulikuwa na viashiria vya rushwa mtego uliandaliwa na kufanikiwa kumtia ofisa huyo mbaroni.

Mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa kesho mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili ya kuomba na kupokea rushwa.