Mwandishi: Grace G. Rweyemam
“Habari Grace. Ninaitwa Ninah, ningependa katika simulizi unazotuma fesibuku, nikupe na wosia wa kaka yangu marehemu, uwaandikie watu. Kabla hajafa aliniomba sana niwambie watu wengi kadiri niwezavyo kile alichotaka wajue. Akaniachia barua ndefu sana aliyoiandika mwenyewe”
Nilisoma ujumbe huo nikastuka na kutamani kujua huo wosia wa marehemu aliotaka uwafikie watu unahusu nini. Nilimpa anuani yangu ya barua pepe na kumuomba aniandikie huo wosia humo, nijue kama kweli ungefaa kuwafikia watu kama ambavyo marehemu alidai.
Nirudi nyuma kidogo, Kuna mdogo wangu yuko katika kundi moja la fesibuku, la wasichana na wanawake, amekuwa akinisimulia visa kadha wa kadha vinavyowatokea wadada wengi walio kwenye ndoa.
Mambo mengi ambayo huwa hunisimulia hunifanya nijue kumbe kweli UKIMWI bado upo na unaua. Kuna kisa fulani aliniambia miezi kadhaa iliyopita, kikanifanya nitamani kama watu wengi zaidi wangeelewa uhalisia wa huu ugonjwa na jinsi unavyowamaliza wengi mpaka leo hii, hata wale wasiotegemea.
Mbaya zaidi kwa sasa ambapo kumekuwa na dawa za kuongeza kinga, wagonjwa wengi wa UKIMWI hawajulikani kwa kuonekana kwa macho, na huo umekuwa mtego kwa watu wengi.
Kuna binti mmoja, nitampa jina la Vero, kwenye hilo kundi ana ndoa ya miaka mitatu na wana mtoto mmoja, aliwahi kufuma jumbe za mapenzi kwenye simu ya mume wake, mwanaume akawa akijitetea na kuomba msamaha, binti akasamehe.
Siku moja binti aliamua kufuatilia namba, alipofuma tena ujumbe wa mapenzi kwa mume wake, akaja kugundua kumbe ni ya jirani yao, cha kumshangaza zaidi huyo jirani yao ni kijana wa kiume.
Binti akachanganyikiwa ndipo akaamua kuomba ushauri kwenye hilo kundi, pasipo kujitaja jina lake, watu wakamshauri asamehe, asimfuatilie mwanaume, wengine wakashauri aachane naye, na kuna waliomshauri akapime na akikutwa salama basi amuache.
Sasa akiwa anafikiria nini cha kufanya, siku mbili baadaye akiwa nyumbani kwake, alitembelewa na jirani yake mwingine nitamuita Siwema. Katika maongezi yule mwanamke Siwema, bila kujua chochote akaanza kuelezea kuwa yule kijana jirani ambaye Vero aligundua kwamba ana mahusiano na mumewe ni shoga na ni muathirika.
Siwema aliongea kwa malalamiko kuwa kuna mtoto wa dada yake (naye ni wa kiume) alikuja kuishi kwake kwa muda wa miezi mitatu akiwa likizo ndefu ya chuo kikuu, kumbe walianzisha mahusiano na yule mvulana. Sasa anadai siku kadhaa zilizopita amegundulika ameathirika, amechanganyikiwa sana kijana pamoja na mama yake.
Siwema alisema alishasikia tetesi hapo nyuma kuwa yule kijana ameathirika, ila hakutilia mkazo sana, mpaka alipogundua amemuambukiza huyo mtoto wa dada yake, kwani kijana baada ya kupimwa na kukutwa na UKIMWI alimueleza mama yake ukweli kuhusu ni wapi anahisi ameutoa.
Akielezea tena Vero kupitia kwa kiongozi (admini) wa hilo kundi, alisema, “Nikiwa bado nawaza kuhusiana na ushauri wenu, nilikuja kugundua kuwa yule kijana anayetembea na mume wangu ni kweli ni shoga na ameathirika.