SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 19 Februari 2018

T media news

Waziri Mkuu Ampa Siku 3 Mkurugenzi Ajiieleze Matumizi ya Milioni 350

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku tatu kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe Bw. Frank Bahati aeleze amepeleka wapi zaidi ya sh milioni 350 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya miradi mbalimbali.

Ametoa agizo hilo jana (Jumapili, Februari 18, 2018) wakati akizungumza na madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe akiwa katika siku ya nne ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.

Waziri Mkuu amesema Serikali haiwezi kuvumia kuona fedha inazopeleka katika halmashauri hiyo kwa ajili ya kugharamia miradi na kulipa madai ya watumishi zinatumika kinyume na maelekezo.

Alisema miongoni mwa fedha hizo ni sh. milioni 451.47 za miradi ya miradi ya maendeleo (CDG), ambapo zilizotumika ni sh. milioni 221.9 tu.” Namtaka Mkurugenzi na Muweka hazina wa Halmashauri hii Bw. Peter Molel tarehe 21 waje Mwanza wanieleze walikopeleka fedha hizo.”

Waziri Mkuu amesema fedha zingine ni sh. milioni 50 za ziizotolewa na Serikali kwa ajili ya kulipa madai mbalimbali ya watumishi kama likizo ambapo zililipwa sh. milioni 13 na zingine hazijulikani zilipo.

Pia Serikali ilitoa sh. milioni 65 za kugharamia mradi wa umwagiliaji wa Bugorola ambazo nazo hazijulikani zilipo pamoja na sh. milioni 84 zilizotolewa kwa ajili ya kulipa motisha kwa walimu ambapo zilizolipwa ni sh. milioni 60 tu.

“Kama mlidhani Ukerewe ni sehemu ya kutafunia fedha za umma mmekosea kwa sababu Serikali haiwezi kuvumia haya, Mkurugenzi umeaminika na kupewa dhamana ya kusimamia rasilimali za umma lakini unafanya tofauti.”

Waziri Mkuu amesisitiza kwamba lazima viongozi hao wahakikishe fedha zinazopelekwa na Serikali katika Halmashauri zao zikiwemo za utekelezaji wa miradi ya afya, elimu, uvuvi zinatumika kama ilivyoelekezwa na si vinginevyo.

Pia Waziri Mkuu amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza asimamie utendaji wa viongozi na watumishi katika  wilaya zote za mkoa huo na kisha kutoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, Bw. John Mongella.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa Halmashauri hiyo wasikubali kugawanywa kwa sababu ya maslahi ya watu ambayo hayana tija kwao na hata kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Waziri Mkuu ameyasema hayo baada ya kubaini kuwepo kwa mgogoro kati ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Bahari pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Bw. George Nyamaha ambao wamekuwa wakiwagawa watumishi.

Amewataka viongozi hao kurekebisha tofauti zao kwa sababu mgogoro wao umesababisha watumishi kugawanyika, hivyo kuwaumiza wananchi wa wilaya ya Ukerewe kwa kushindwa kuwahudumia vizuri jambo ambalo halikubaliki.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMAPILI, FEBRUARI 18, 2018.