Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Michael Mteite, jana alitaja maswali matatu yaliyomfanya afikie uamuzi wa kuwatia hatiani Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na mwenzake.
Sugu na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga, walihukumiwa kifungo cha miezi mitano jela kila mmoja baada ya kukutwa na hatia ya kutoa lugha za fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mteite alisema Mahakama imejiridhisha kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri ulikuwa ni wa kweli kwani waliona na kusikiliza maneno yalitolewa.
Hakimu Mteite alisema kabla ya kufikia uamuzi wake, hata hivyo, Mahakama imeona viini vitatu ambavyo vilitengeneza maswali katika kesi hiyo.
Aliyataja maswali hayo kuwa ni je, maneno yaliyotolewa na washtakiwa kweli yalikuwa ni ya fedheha dhidi ya Rais? Mlengwa katika shauri hilo ni Rais John Magufuli kweli? Na je, washtakiwa walitoa maneno hayo?
Katika dhana hiyo, Hakimu Mteite alisema kutokana na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri ni kweli washtakiwa walitoa maneno hayo, na kwamba waliyekuwa wanamsema ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Haya maneno ya washtakiwa kuwa huwezi kupendwa kwa ‘kumshuti’ Lissu, kumteka Ben Saanane, watu kuuawa mchana kweupe na kufungwa kwenye viroba, Rais anatubadilishia aina ya kututawala… ni ya kitaifa na yanamhusu Rais Magufuli ambaye ndiye mtawala,” alisema Hakimu Mteite.
Hakimu huyo alisema ushahidi wa upande wa Jamhuri ambao ulitolewa na William Nyakomago na Joram Magova ulikuwa na uzito kwa sababu ni polisi ambao walikuwepo eneo la tukio na sauti iliyotolewa mahakamani kama kielelezo ilikuwa ni ya washtakiwa.
Aidha, Hakimu Mteite aliiambia mahakama ushahidi uliotolewa na upande wa utetezi ulikuwa hauna nguvu.
Alisema mshtakiwa namba mbili, Masonga, alikana mbele ya mahakama kuwepo kwenye mkutano siku hiyo lakini hakuna kielelezo alichotoa mahakamani hapo kuthibitisha; hivyo mahakama haikutambua utetezi huo.
Kabla ya Hakimu Mteite kutoa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Joseph Pande aliiomba mahakama kuwapa adhabu kali washtakiwa ili iwe funzo kwa wengine.
Wakili wa utetezi, Peter Kibatala aliiomba mahakama kuwapunguzia adhabu washtakiwa kutokana na majukumu ya kibunge na kifamilia walionayo.
Pia alisema adhabu kali itaathiri shughuli za kibunge na za maendeleo kwa wananchi wa Jimbo la Mbeya Mjini, na kwamba washtakiwa walishakaa mahabusu kwa takribani mwezi mmoja mpaka mahakama ilipotoa dhamana.
Wakili Kibatala alidai pia sheria inaruhusu washtakiwa kama wamekutwa na hatia wapatiwe adhabu mbadala, ikiwemo faini na kueleza mahakama haijaonyesha kosa hilo lina uzito kiasi gani. Wakili Kibatala alisema pia hakuna kumbukumbu ya washitakiwa kufanya kosa hilo awali.
“Rais ni mwanasiasa kama ilivyo kwa washtakiwa,” alisema Kibatala, “hivyo maneno yaliyotolewa ni ya kisiasa na yachukiliwe hivyo hivyo”.
“Ni kweli Mlengwa alikuwa ni Rais Magufuli (lakini) hakuna ushahidi unaoonyesha hadhi ya Rais imeshuka.”
Awali wakati wa usikilizaji shauri hilo, washtakiwa hao walikana kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais Magufuli na kwamba sauti zilizokuwa zimetolewa kortini kama kielelezo si zao.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya ilianza kusikiliza kesi hiyo Januari 16, mwaka huu. Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Sugu na mwenzake walitumia lugha za fedheha dhidi ya Rais John Magufuli Desemba 30, mwaka jana katika viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge.