JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani imesema kuwa haitawapa nafasi ya kuwa viongozi baadhi ya wanachama waliokisaliti chama wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka juzi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Bagamoyo mwenyekiti wa jumuiya hiyo Abdul Sharifu alisema kuwa kwa kuwa mwaka huu ni wa uchaguzi wa chama na jumuiya zake wasaliti hawatapata nafasi.
Sharifu alisema kuwa katika kipindi cha uchaguzi mkuu uliopita baadhi ya viongozi na wanachama walikisaliti chama na kusababisha kukosa kura au wagombea wake kushindwa.
“Kwa sasa haali ya kisiasa iko vizuri ndani ya chama na tunaendelea vizuri kwa sasa tunaendelea na maandalizi ya uchaguzi ndani ya chama na jumuiya zetu tutahakikisha wagombea wetu wanakuwa ni wale wenye uwezo na moyo na chama tutaachana na wale ambao walitusaliti kwani taarifa zao tunazo,” alisema Sharifu.
Alisema kuwa wale waliokipigania chama kwa hali na mali tutahakikisha ndiyo wanaopata nafasi za kuwa viongozi na kuachana na mamluki ambao wanatusaliti.
“Kwa upande wa mabadiliko yaliyofanya na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk John Magufuli ya kuondoa baadhi ya nafasi, ni kuleta ufanisi katika uongozi na kuleta uwajibikaji ndani ya chama,” alisema Sharifu.
Kwa upande wake Mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya Bagamoyo, Amiry Mkangata alisema kuwa kupunguzwa kwa baadhi ya nafasi kutasaidia kuleta utumishi bora ndani ya chama.
Mkangata alisema kuwa baadhi ya viongozi wa CCM walikuwa hawajui wajibu wao ambao kazi yao kubwa ni kuisimamia serikali ili itekeleze wajibu wake kwa sawa na sera za chama.
Aliwataka wananchi kuvumilia mabadiliko anayoyafanya Rais kwa kipindi hichi kwani baadaye mambo yatakuwa mazuri na hali itakuwa kama kawaida.