Wizara ya Mambo ya Ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza majina ya wabunge waliochaguliwa kuziwakilisha dini zenye wafuasi wachache bungeni.Kwa mujibu wa matokeo rasmi yalioyotangazwa jana Jumatatu, Siamak More Sedeq ameibuka mshindi kuwa mwakilishi wa Mayahudi hapa nchini, kwa kupata kura 2,449. Esfandiyar Ekhtiyari ametangazwa mshindi wa jamii ya Wazartoshti baada ya kupata kura 3,966. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran imetangaza kwamba, Younatan Betkolia amechaguliwa kuwawakilisha bungeni watu wa jamii za Assyria na Chald kwa kupata kura 2,212. Georgik Abrahamian ndiye amechaguliwa kuwawakilisha Wakristo wanaoishi kusini mwa Iran kwa kupata kura 2,290 huku Karen Khanleri akichaguliwa kuwawakilisha wafuasi wa dini za wachache wanaoishi kaskazini mwa nchi, kwa kura 8,631.Kwa mujibu wa Sura ya 12 ya Sheria za Uchaguzi, wafuasi wa dini za wachache nchini Iran wana haki zote za kiraia na kijamii ikiwemo haki ya kuwa na mwakilishi wao bungeni. Kati ya viti 290 vwa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu yani Bunge la Iran, viti vitano vimetengewa wawakilishi wa dini za wachache nchini.Hii ni katika hali ambayo, Ali Larijan, Spika wa Bunge la Iran amesema kuwa mahudhurio makubwa ya wananchi wa Iran katika uchaguzi uliofanyika Ijumaa iliyopita hapa nchini yamezidisha hadhi ya Iran katika nyanja za kimataifa. Asilimia 62 ya wananchi milioni 55 waliotimiza masharti ya kupiga kura walishiriki katika uchaguzi huo, wa Bunge la 10 la Jamhuri ya Kiislamu na wa 5 wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu.