Baraza Kuu la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) jana Jumamosi Aprili 7, 2018 limetoa tamko lenye mambo saba, likiwemo la kupinga uamuzi wa Serikali kuwafuta kazi watumishi wake wenye elimu ya darasa la saba.
Akisoma tamko hilo mbele ya wajumbe wa baraza kuu la Tucta katika mkutano wa baraza hilo uliofanyika mkoani Morogoro mwenyekiti wa Tucta, Tumaini Nyamhokya alisema uamuzi huo wa Serikali si sahihi na hivyo wametaka watumishi hao kurejeshwa kazini.
Alisema baraza limesikitishwa na uamuzi wa kuwaondoa kazini watumishi wa umma na taasisi zinazopokea ruzuku kutoka serikalini.
Nyamhokya alisema uamuzi huo si wa kisheria ikizingatiwa kuwa watumishi hao waliajiriwa kwa kufuata taratibu halali za ajira.
“Kwa hiyo Tucta tunaitaka serikali kutengua uamuzi wake na kuwarudisha watumishi hao kazini bila kupoteza haki zao za kiutumishi kwa kipindi chote,” alisema.
Mambo mengine sita yaliyopo katika tamko hilo wanayotaka yafanyiwe kazi ni; ongezeko la mishahara, kodi ya mishahara (PAYE), kupandishwa madaraja na vyeo kwa watumishi wa umma, malimbikizo ya mishahara kwa wafanyakazi na watumishi kwa baadhi ya taasisi, ucheleweshwaji wa malipo ya wastaafu kwa baadhi ya mifuko ya hifadhi ya jamii na uamuzi wa Serikali kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii.