Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa imeipiga kalenda kesi ya mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi (TSNP), Abdul Nondo hadi Jumatatu kutokana na mabishano makali ya kisheria yaliyotokea kortini hapo kati ya pande mbili za utetezi na Jamhuri.
Akiahirisha kesi hiyo, Hakimu Mkazi John Mpitanjia alisema anajipa muda kwa lengo la kupitia sheria kuhusiana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na shahidi wa pili; kwamba kielelezo chake kipokelewe na mahakama ama la.
Upande wa uetetezi ukiongozwa na wakili Jebra Kambole akisaidiwa na Chance Luwoga, uliomba mahakama kutopokea hati ya upekuzi kwa madai ina mkanganyiko wa majina na kwamba ni watu wawili tofauti.
Aidha, utetezi ulipinga hati ya uchunguzi kuwa imekosewa jina la mshitakiwa kwani badala ya kuandika Abdul Mahamud Omary Nondo imesajiliwa kwa jina la Mahmud Omary Nondo.
Upande huo uliomba kutupiliwa mbali kwa nyaraka hiyo ambayo upande wa Jamhuri ukiongozwa na wakili wa serikali, Alex Mwita akisaidiwa na Pianzia Nchemba umesema cha muhimu ni ujumbe uliopo ndani.
Mwita alisema huenda nondo alitoa majina mawili tofauli kwa sababu alihojiwa na watu wawili tofauti.
Hoja ya tatu iliyotolewa na upande wa utetezi ni kwamba ilikuwaje Koplo John kutumia kifungu cha 10 (3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA)Sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kuthibitisha waraka huo ili hali kabla alisajili kwa kutumia kifungu cha 34 (b) cha Sheria ya Ushahidi.
Awali, shahidi wa kwanza ambaye ni E.32328 Koplo Salim aliiambia mahakama kwamba Nondo aliwasili kituo cha polisi majira ya moja usiku na kuchukuliwa maelezo ya awali.
Alidai Nondo alisema amefika kituoni kutoa malalamiko ya kutekwa na watu wasiojulika na kutelekezwa katika Kiwanda cha Pareto Pct Mafinga.
Kolpo Salim aliiambia mahakama kuwa Nondo aliiambia Polisi kwamba alitekwa jijini Dar es Salaam na kusafirishwa hadi Mafinga Iringa na ndipo alimkabidhi kwa mpelelezi Koplo John mwenye namba E.7665 ambaye ni shahidi wa pili katika kesi hiyo, ili aweze kumchukua maelezo kwa kina kuhusiana na malalamiko yake.
Hata hivyo, mahakama ilipokea vielelezo ambavyo Nondo alivikabidhi Kituo cha Polisi Mafinga ambavyo ni kompyuta mpakato aina ya Dell, kadi ya mawasiliano (bussness card), kadi ya benki, simu ya kiganjani aina ya Itel na kitambulisho cha chuo.
Awali, Hakimu Mpitanjia alisema kabla ya mashahidi kutoa ushahidi wao inabidi mtuhumiwa kusomewa mashataka yake yanayomkabili na Nondo alikana mashtaka hayo.
Jamhuri imekusudia kuleta mashahidi watano zaidi ambapo jana ni mashahidi wawili tu waliopanda kizimbani kutokana na kutofikia muafaka baada ya pande mbili hizo kunyukana kwa kutumia vifungu vya sheria.
Jamhuri imekusudia kuwaleta pia kutoa ushahidi Koplo Salum, Veronica Fredy ambaye ni mpenzi wake Nondo, Alphonce Mwamule, Koplo Abdulkadir na mtu kutoka kampuni ya simu za mkononi ya Tigo.
Nondo ameshitakiwa kwa makosa mawili ya kuchapisha taarifa za uongo kwa njia ya kompyuta na kutoa taarifa za uongo kwa mtumishi wa umma ambaye ni askari polisi Koplo Salim wa Kituo cha Polisi Mafinga wilayani Mufindi.
Ilidaiwa kwamba Machi 7, mwaka huu akiwa Ubungo jijini Dar es Salaam, mshitakiwa alitenda kosa la kuchapisha taarifa za uongo kwa njia ya kompyuta akitumia simu ya kiganjani yenye No. 0659366125 kinyume cha Sheria ya Makosa ya Mtandao na kusambaza katika mitandao ya kijamii.