Diwani wa kata ya Gwarama wilayani Kakonko mkoani Kigoma, Bw.Elia Michael amepinga vikali agizo la Rais JPM la kuwataka polisi kukamata wananchi wa kijiji kizima kwenda kufyeka bangi ikiwa kijiji chao kitabainika kuwa na shamba la bangi.
Diwani huyo amewaeleza wananchi wake kuwa agizo hilo ni batili na ni kinyume na sheria mbalimbali na katiba ya nchi, ikiwemo sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (Criminal Procedure Act, Cap 20) na sheria ya polisi (Police Force and Auxiliary Services Act, Cap.322) zinazozuia polisi kukamata mtu asiye mtuhumiwa wa kosa lolote, na kusisitiza kuwa ni kosa kuadhibiwa kwa kosa la mtu mwingine.
Ameeleza pia agizo hilo ni kinyume na utaratibu wa utendaji wa serikali za mitaa, kwani serikali ya kijiji haiwajibiki kwa jeshi la polisi, bali jeshi la polisi linawajibika kwa serikali ikiwemo ya kijiji. "Polisi haina mamlaka ya kuiagiza serikali ya kijiji, ila serikali ya kijiji ina mamlaka ya kuwaagiza polisi" amesema na kuwataka washauri wa JPM kusoma sheria ya serikali za mitaa ya mwaka 1982.
_
"Kila kijiji kina serikali yake, inayofanya kazi kwa mujibu wa sheria. Haiwajibiki polisi. Lazima serikali hizo ziheshimiwe. Kama kutatokea shamba la bangi kijijini, serikali ya kijiji ichukue hatua. Ikiwa mtuhumiwa atashindwa kubainika, viongozi wa kijiji husika wawajibike, lakini sio kukamata kila mtu hadi viongozi wa dini kwa jambo ambalo hawahusiki nalo." Amesema Elia.
_
"Kama kwenye vijiji vya kata yangu ya Gwarama, ikaonekana shamba la bangi wananchi hawatafyeka bangi hiyo. Mark my words HAKUNA MWANANCHI ATAKAYEKAMATWA KWENDA KUFYEKA BANGI KWENYE KATA YANGU" amesisitiza Elia.
_
"Ni jukumu la vyombo vya usalama kuteketeza mihadarati. Mbona wakikamata aina nyingine ya dawa za kulevya kama cocaine hawaiti wananchi wakateketeze, ila bangi wanalazimisha wananchi wote washiriki kuteketeza? Hii si sawa. Ikitokea bangi kwenye kata yangu polisi ndio watafyeka bangi hiyo. Hakuna atakayeweza kuwalazimisha wananchi wakafyeke." Amesema diwani huyo mwenye umri mdogo kuliko madiwani wote nchini, ambaye pia ni mhitimu wa chuo kikuu UDSM.!