RAIS Donald Trump amemwondoa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson, na amepanga kumteua Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la nchi hiyo (CIA), Mike Pompeo, kuchukua nafasi ya waziri huyo.
Maofisa wa Ikulu ya Marekani wamesema hatua hiyo ya rais huyo ni kutaka kuonyesha mabadiliko makubwa katika timu ya maofisa wa masuala ya usalama wa taifa katika juhudi zake anazozifanya, yakiwemo mazungumzo na Korea ya Kaskazini.
Ijumaa wiki iliyopita, Trump alimtaka Tillerson aachie ngazi, ambapo waziri huyo alikatisha safari zake barani Afrika jana na kurejea Washington. Kutoelewana kati ya Trump na Tillerson kumekuwepo kwa miezi mingi ambapo ilimbidi rais huyo kufikia uamuzi huo alioufanya.
Sababu hasa ya kutoelewana huko haifahamiki, lakini imeonekana kwamba wawili hao wamekuwa wakitofautiana katika sera za masuala la zana za nyuklia kuhusisna na Iran. Hata hivyo, msemaji wa Tillerson alisema kwamba waziri huyo alikuwa na dhamira ya kuendelea katika nafasi hiyo na hakuelewa sababu yoyote iliyosababisha ang’olewe.
Rex Tillerson ameondolewa madarakani ikiwa ni siku moja tangu aondoke nchini Kenya alipokuwa kwenye ziara ya kikazi na kuelekea Ghana ambako alikuwa anaendelea na ziara yake Barani Afrika.
Aidha, Trump amemteua Gina Haspel kama mwanamke wa kwanza kuwa Mkurugenzi wa CIA. Tillerson aliapishwa Februari 2017 kushika wadhifa huo