Mara baada ya kumwagana na mama watoto wake, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ kisha kumuahidi mama yake kuwa mwaka huu lazima afunge ndoa, staa wa Afro-Pop, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, ameibua gumzo la aina yake juu ya ni nani atakayemuoa huku warembo kadhaa wakianikwa.
Machi 8, mwaka huu ilikuwa ni Siku ya Wanawake Duniani ambapo Diamond alitumia siku hiyo kuwatakia heri wanawake mbalimbali wakiongozwa na mama yake, Sanura Kassim ‘Sandra’, zilipendwa wake watatu, Zari, Wema Sepetu na Hamisa Mobeto.
Kufuatia kauli yake hiyo, kuliibuka tafrani kwenye mitandao ya kijamii ambapo warembo kadhaa walihusishwa kuwa huenda mmojawapo ‘akaokota dodo chini ya mpera’ kwa kuolewa na Diamond.
Gazeti hili la Risasi Mchanganyiko linakuletea uchunguzi na uchambuzi wa kina juu ya uwezekano wa mwanamke ambaye ataolewa na jamaa huyo;
Pamoja na kwamba Zari hataki kusikia ishu ya msamaha, lakini uchunguzi wetu ulibaini kwamba, endapo wawili hao wataamua kusameheana kwa kusikiliza maombi ya mashabiki wao ambao wanataka warudiane kisha wakaweka ustaa pembeni na kukubali kusameheana, basi wanaweza wakafunga ndoa.
Zari anabebwa na kigezo cha kuwa boss lady. Kwamba hamtegemei Diamond kwa lolote kwani bibiye pesa imemtembelea, jambo ambalo kwa Diamond anaona atapata mteremko wa malezi ya kifamilia hivyo yeye atabaki kujikita kwenye ishu ya kusaka tu mafanikio kupitia muziki wake.
Hata hivyo, ilibainika kwamba, uwezekano wa Diamond kumuoa Zari ni mdogo kwa kuwa alishapata alichokitaka yaani watoto wawili, Tiffah na Nillan na mbaya zaidi bado suala la umri wa Zari wa miaka 36 ni tatizo kwani ndiyo kwanza Diamond ana 26 na damu inachemka.
Mobetto.
Hamisa Mobeto na Diamond hawakuanza mapenzi yao juzi. Kwa mujibu wa Mobeto, wamedumu kwenye uhusiano yapata miaka tisa kabla ya kujaliwa mtoto mmoja wa kiume, Prince Dully baada ya Diamond kuchepuka kutoka kwa Zari.
Inaaminika kuwa, uhusiano wa Mobeto na Diamond ulianza hata kabla hawajawa mastaa hivyo ni vigumu kuwatenganisha kwani wametoka mbali na wanajua kuvumiliana kwa mengi.
Hata hivyo, suala la Diamond kumuoa Mobeto lina uwezekano mdogo mno kwani walichokitaka ni mtoto na tayari wamempata huku mrembo huyo akiwa ameshazaa na bosi maarufu wa redio jijini Dar. Inaaminika alizaa na bosi akiwa bado yumo ndani ya uhusiano na Diamond hivyo kuna ishu ya usaliti ambayo inapunguza asilimia za wawili hao kufunga ndoa.
WEMA
Baada ya Diamond kumwagana na Wema yapata miaka minne iliyopita alitua kwa Zari. Uchunguzi wetu ulibaini kwamba, tangu Wema aachane na Diamond hajawahi kutulia na mwanaume huku kukiwa na shinikizo kubwa kutoka
kwa mashabiki wao wakiomba usiku na mchana warudiane na wafunge ndoa, japokuwa hakuna aliye tayari kwa hilo.
Hata hivyo, uwezekano wa Diamond na Wema kufunga ndoa haupo kwa sababu wameshasema kwamba, hakuna mapenzi tena kati yao badala yake wapo kikazi zaidi.
Wema atakuwa miongoni mwa watangazaji wa Wasafi TV ambapo anamchukulia Diamond kama bosi wake.
TUNDA
Video queen Tunda Sebastian, anapenda kujiita Boss Baby ili aonekane ana pesa. Naye anatajwa kuwa mmoja wa warembo wanaomchanganya Diamond kutokana na uzuri na taarifa kuwa ‘eti hajatumika sana’ ukilinganisha na wengine. Pia Tunda anabebwa na utoto na kutozaa hivyo Diamond anadaiwa kutaka kuzaa naye ili amwachie ‘chata’ kama alivyofanya kwa Mobeto.
Kufuatia hali hiyo, Tunda amekuwa ‘kiguu na njia’ kila anapokatiza Diamond naye anakuwa nyuma kuanzia safari za Rwanda, Kenya na Afrika Kusini.
Hata hivyo, uwezekano wa Tunda kuolewa na Diamond inasemekana ni kiduchu mno kwa kuwa Tunda hana pesa kama Zari pamoja na kwamba wanapendana kama makinda ya njiwa.
Huddah ‘Boss Chick’
Kuna taarifa kuwa, endapo Diamond atataka kutoka nje ya Tanzania, basi anaweza kujituliza nchi jirani ya Kenya. Mrembo Huddah Monroe wa Kenya amekuwa kwenye mkwaruzano wa mara kwa mara na Zari baada ya kugundua kuna kinachoendelea kati ya mrembo huyo na Diamond.
Kama ilivyo kwa Zari, Huddah anayejiita Boss Chick ni mwanamuziki na mjasiriamali ambaye huvuna mkwanja mrefu kwa kulipwa kwa kuonekana kwenye matukio makubwa.
Mbali na Kenya, kuna taarifa kuwa, hivi karibuni Diamond alitangaza kukita mizizi nchini Rwanda ambapo aliahidi kununua nyumba na kujenga kiwanda nchini humo. Wataalam wa mambo wanasema, kutokana na uzuri wa warembo wa Rwanda ambao ni warefu kama twiga, ni vigumu kwa Diamond kuchomoka hivyo kuna uwezekano wa atakayeolewa akatoka nchini humo.
MSHINDI BBA Dillish Mathews
Uchunguzi huo pia ulibaini kwamba, endapo Diamond atataka kutoka nje ya Tanzania na Afrika Mashariki, basi mrembo kutoka Namibia, Dillish Mathews ambaye ni mshindi wa Big Brother Africa mwaka 2013 anaweza kutwaa nafasi ya kuwa mke wa Diamond.
Dillish anatajwa kuwa miongoni mwa wanawake waliokuwa wakimnyima Zari usingizi kutokana na kuwepo kwa tetesi za muda mrefu kwamba wanatoka kimapenzi japokuwa ilikuwa ni kwa siri kubwa.
Mwishoni mwa mwaka jana, Diamond na Dillish waliripotiwa kuonekana wakijiachia kwenye Visiwa vya Zanzibar katika hoteli ya kifahari ya La Gemma.
Dillish anabebwa na vigezo vingi. Moja, ni mwanamuziki kama yeye na ni hosti wa vipindi vya runingani (television personality) kama ilivyo kwa Zari, Wema na mtangazaji Peniel Mungilwa ‘Penny’ ambaye naye aliwahi kuwa mpenzi wa Diamond.
Kigezo kingine kikubwa ni kwamba, Dillish ni boss lady kwani baada ya kuibuka Mshindi wa BBA alilamba Dola za Kimarekani laki tatu (300,000) zaidi ya shilingi milioni 600 za Kibongo ambazo amewekeza kwenye miradi mbalimbali ikiwemo migahawa nchini kwake, Namibia na Afrika Kusini.
Pia ana jina kubwa Afrika na ni kifaa matata kama Wema.
Hata hivyo, hakuna uhakika kwa asilimia mia moja kuwa ndiye wa kuolewa, lakini kwa kuwa ana mkwanja kama Zari, anaweza ‘kuokota dodo’ kwa Diamond kwani kuna madai mazito kwamba ‘eti anapenda kitonga, ganda la ndizi au mteremko’.
DADA ZAKE
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, dada zake Diamond, Esma Khan ‘Esma Platnumz’ na Mwanahawa Abdul ‘Queen Darleen’ walisema kuwa, hawawezi kumpangia kaka yao huyo juu ya mke atakayetaka kumuoa.
“Mimi yeyote atakayeletwa ni wifi yangu,” alisema Esma.
“Diamond haniingilii kwenye mambo yangu ya uhusiano na mimi siwezi kumpangia, yeyote atakayemuoa kwetu ndiye huyohuyo,” alisema Queen Darleen
DIAMOND ANASEMAJE?
Katika mazungumzo na gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita juu ya atakayemuoa, Diamond alisema kuwa, hakumtaja jina mrembo yeyote, lakini ni lazima mwaka huu afunge ndoa.
“Nipo busy na uzinduzi wa albam yangu ya A Boy From Tandale kwa wiki kama mbili hivi, nikitulia tutazungumza hilo. Lakini sijataja jina lolote,” alisema Diamond.