Ukiwa hauna pesa unaweza ukajiona wewe ndiye mtu mwenye matatizo pengine kuliko watu maarufu unaowaona kila siku kwenye runinga au kuwasikiliza redioni, lakini ukweli ni kwamba maisha hayapo hivyo kila mtu anachangamoto zake. Hii imedhihirishwa na mtangazaji nguli wa kituo cha Citizen TV, Swaleh Mdoe ambaye ametangaza kuuza figo yake moja ili aweze kulipa madeni yanayomkabili.
Swaleh Mdoe ambaye amejipatia umaarufu nchini Kenya kupitia kipindi cha ‘Tafakari na Babu’ cha Citizen TV kinachoruka kwa lugha ya kiswahili amesema anauza figo yake kwa shilingi milioni 1 za Kenya ambayo sawa na milioni 23 za kitanzania.
Msomaji huyo nguli wa taarifa ya habari ya Citizen TV leo Ijumaa Februari 16, 2018 akifanya mahojiano na kituo cha Radio cha Ghetto FM cha Jijini Nairobi nchini Kenya, amesema kuwa kwa sasa yupo katika mtikisiko wa kiuchumi kwani anadaiwa fedha nyingi ndiyo maana amechukua maamuzi hayo.
“Nimejitafakari kwa kina mimi na daktari wangu hadi kuchukua maamuzi ya kutangaza kuuza figo yangu moja, Kuna mambo hayapo sawa kiuchumi kwa upande wangu nataka niyamalize mwenyewe hivyo natangaza kuuza figo yangu kwa yeyote anayehitaji asisite kunitafuta kupitia 0722-733130. Nataka nifanye hili haraka na nitatoa matangazo mengine kwenye magazeti,“amesema Swaleh Mdoe.
Hata hivyo, amesema ingawaje ni mtu maarufu nchini Kenya hataki kutangaza michango watu wamchangie kwani anaona atawabunguzi watu ambao hawahusiki na madeni hayo.
“Sitaki kuwabughuzi watu wengine kwa sababu ya umaarufu wangu, nadhani figo moja inatosha kulipa madeni yangu yote na mwili wangu utakuwa na afya kama nilivyo sasa,“amesema Mdoe na kuwataka Wakenya wenye matatizo ya uhitaji wa figo wamtafute.