SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 12 Februari 2018

T media news

Hizi ndizo faida za kuwa na Kitambulisho cha Taifa

Kati ya vitu muhimu ambavyo mwananchi yeyote anapaswa kuwa navyo kwa sasa ni kitambulisho cha Taifa.

Umuhimu huo hautokani tu na kumtambulisha mwananchi kuwa ni raia wa Tanzania tu, bali sasa ndicho kitakachomuwezesha kusajili kampuni, kuomba hati ya kusafiria na kupata cheti cha kuzaliwa.

Kitambulisho hicho kinatolewa na Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA), ni mkakati wa serikali kuhakikisha kuwa kila Mtanzania mwenye miaka 18 na kuendelea anakuwa nacho ili kumwezesha kupata huduma muhimu.

Januari 31, Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji, Dk Anna Makakala alisema ili Mtanzania apate hati ya kusafiria ni lazima awe na kitambulisho cha Taifa na si vinginevyo.

Wakati Uhamiaji ikisisitiza kitambulisho hicho, Wakala wa Usajili wa Kampuni (BRELA) nao ulitangaza kuanza kusajili kampuni kwa njia ya mtandao huku kigezo kikuu ili kusajili kikiwa ni kitambulisho cha Taifa.

Taarifa ya Brela iliyotolewa inasema, ambao hawajasajiliwa kupata vitambulisho, wataendelea kusajiliwa kwenye ofisi za NIDA.

Kwa upande wao, Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (RITA) nao ulisema kuanzia sasa wananchi wananweza kutumia kitambulisho cha Taifa au kitambulisho cha mpiga kura ili kupata cheti cha kuzaliwa.

Baadhi ya mambo muhimu kuhusu kitambulisho hicho ni kusaidia kuongeza wigo wa mapato ya serikali, kumtambua mhusika kirahisi anapohitaji kupatiwa huduma katika taasisi mbalimbali kama vile benki, taasisi za mikopo na huduma za afya.

Pia, vitarahisisha kuwatambua wakwepaji wa kurejesha mikopo kutoka kwenye benki na asasi mbalimbali za fedha nchini, kuweka kumbukumbu za matukio ya uhalifu katika daftari la kumbukumbu la kielektroniki n.k.

Kitambulisho hicho kiwawezesha pia kumtambua mtu anapofanya biashara au shughuli nyingine kwa kutumia majina tofauti. Vitahakikisha kuwa mtu anapata stahiki zake katika jamii.

Kwa mfano, kupata malipo ya pensheni, haki za matibabu, haki ya kujiunga na masomo ikiwa ni pamoja na stahili zozote ambazo raia wa Tanzania anastahili kupata kirahisi kwani kupitia Kitambulisho cha Taifa, mwananchi atatambulika kirahisi (nani ni nani, yuko wapi na anafanya nini).

Umuhimu mwingine ni kuondoa watumishi hewa kwenye mfumo wa malipo ya mishahara ‘payroll’ ya serikali, kuimarisa utendaji kazi serikalini kwa kuwa na kumbukumbu sahihi za watumishi na malipo ya stahili zao, hasa pale wanapostaafu.

Pia, vitarahisisha kazi ya kuhesabu watu (sensa), kurahisisha kazi ya kuhuisha daftari la wapigakura, kazi ambayo kwa sasa hufanyika mara mbili kabla ya uchaguzi mkuu.