SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 24 Januari 2018

T media news

Sababu zilizopelekea Halmashauri ya Jiji Dar kuihamisha stendi ya Ubungo

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imetenga shilingi bilioni 8.5, kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi wanaoishi eneo la Mbezi luis, ambalo linatarajiwa kujengwa kituo kipya cha mabasi yaendayo mikoani.

Kituo hicho kinahamishwa kutoka eneo la ubungo Terminal na kupelekwa Mbezi luis huku stendi ya Ubungo ikitafutiwa shughuli nyingine kwa ajili ya kuimarisha uchumi.

Akizungumza jana katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam, Mkurugenzi wa jiji hilo, Spola liana alisema utaratibu wote umekamilika kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi hao ili wapishe eneo hilo kwa ajili ya shughuli hiyo.

Spola alisema utaratibu wa wananchi kulipwa fedha zao ukikamilika, kitakachofuata ni kuanza kwa ujenzi wa kituo hicho.

“Kituo hicho kitakuwa na nafasi kubwa na ulinzi uliokamilika kwa wananchi wetu, ndio maana tumeona ni vyema kituo hicho kuhamishiwa Mbezi Luis kwa maendelezo zaidi,” alisema Spola.

Wakati huo huo, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Huduma za Jamii ya baraza hilo wameiomba Halmashauri ya Jiji kurudisha fedha za halmashauri walizotoa kwa ajili ya ujenzi wa machinjio ya kisasa.

Akizungumza katika kikao hicho, Meya wa Temeke, Abdallah Chaurembo aliitaka halmashauri hiyo kurudisha fedha hizo, ambapo kila halmashauri ilitoa shilingi milioni 500, kwa ajili ya ujenzi wa machinjio ya kisasa.

Chaurembo alisema lengo ka fedha hizo lilikuwa ni ujenzi wa machinjio lakini hayakujengwa, badala yake ilitaka kuanzishwa kampuni ya usambazaji nyama na hilo halikutekelezwa.

“Hadi sasa hakuna ujenzi wa machinjio na hakuna kampuni ya nyama inayofanya kazi, hivyo ni vyema fedha hizo zingerudishwa ili zifanye shughuli zingine za kimaendeleo.” alisema.

Meya wa Kinondoni, Benjamin Sitta alitoa ushauri kwa halmashauri hiyo kufanya manunuzi ya magari kwa ajili ya kukusanya taka katika wilaya zake.

Sitta alisema jiji la Dar es Salaam litakuwa jij la utaliii hivyo lazima usafi uimarishwe katika kila wilaya.

“Hakuna jiji linaloingiza mapato makubwa isipokuwa Dar es Salaam, hivyo usafi uimarishwe zaidi, ili watalii kadiri wanavyotembelea Dar es Salaam iendelee kusifika nje ya nchi,” alisema Sitta.