Mahakama ya Rufaa Tanzania imekubali maombi ya Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Wananchi (CUF) inayomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho,Maalim Seif Sharif Hamad katika shauri Namba 43/01/2017 kuhusu kumkataa Jaji Kihiyo kusikiliza shauri la msingi.
Taarifa hiyo ya maamuzi ya mahakama ya Rufaa, imetolewa mapema leo Disemba 22, 2017 kwa vyombo vya habari na Naibu Mkurugenzi wa Habari CUF, Mbarala Maharagande.
“Mahakama ya Rufaa imeipa ushindi Maombi ya Bodi ya Wadhamini ya CUF chini ya Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad katika shauri Namba 43/01/2017 (From Civil Application No.23/2017) kuhusu kumkataa Jaji Kihiyo kusikiliza shauri la msingi tajwa hapo juu.
“Shauri hili ndilo linalohoji uhalali na mamlaka ya Msajili wa vyama vya siasa nchini Jaji Francis Mutungi kumrejesha Lipumba katika nafasi ya Uongozi ndani ya CUF baada ya kujiuzulu na kukubaliwa kujiuzulu kwake na Mkutano Mkuu wa Taifa wa CUF uliofanyika katika ukumbi wa Blue Pearl, Ubungo Plaza Tarehe 21 August, 2017,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Jaji wa Mahakama ya Rufaa , Jaji Musa Kipenka amekubaliana na hoja za Mawakili Wasomi wa CUF Halfani Daimu, Juma Nassoro na Hashimu Mziray walizozitoa Mbele ya Mahakama hiyo.
Maharagande amesema, maamuzi hayo yanaipa nafasi mahakama kuu kuendelea kusikiliza shauri hilo ambalo Msajili wa Mahakama Kuu ameshalipangia jalada ambalo linasikilizwa mbele ya Jaji Wilfred Ndyansobera.