SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 8 Novemba 2017

T media news

Takukuru Yajitosa Uchunguzi Bodi ya Mikopo

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inafanya uchunguzi dhidi ya vigogo na maofisa wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) wanaotuhumiwa kutafuna mabilioni ya shilingi kutokana na mbinu mbalimbali ikiwamo ya kujilipa posho ya ukarimu, imefahamika.

Agosti 31, mwaka jana, wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ikipitia taarifa za fedha za bodi hiyo kwa mwaka 2014/15, ilibainika imetumia Sh. bilioni 15 kwa shughuli za uendeshaji huku kiasi kikubwa kikiwa posho.

Kutokana na 'madudu' hayo, kamati hiyo iliitaka bodi kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuhakikisha ulipaji wa posho
unazingatia sheria na miongozo ya serikali.

Kabla ya kupitiwa kwa taarifa za fedha za bodi hiyo na PAC Februari 16, mwaka jana, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.
Joyce Ndalichako, alitangaza kusitisha mkataba wa ajira wa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, George Nyatega, pamoja na kuwasimamisha kazi wakurugenzi watatu kutokana na kile alichokieleza siku hiyo kuwa matatizo ya kiutendaji na matumizi mabaya ya fedha za umma yanayofanyika ndani ya bodi hiyo.

Prof. Ndalichako alisema taasisi hiyo imeonyesha utendaji usioridhisha kiasi kwamba kumekuwa na matatizo mengi na yanayojirudiarudia kwa wateja wao.

“Mikopo kwa wanafunzi imekuwa ikichelewa kuwafikia bila sababu za msingi kiasi kwamba imejengeka taswira kwa wanafunzi kwamba hadi walalamike wizarani ndipo matatizo yao yashughulikiwe, hivyo tatizo si ukosefu wa fedha bali ni uzembe wa watendaji katika kuwapatia wanafunzi mikopo yao kwa wakati," Prof. Ndalichako alisema.

Watumishi wa bodi hiyo waliosimamishwa kazi siku hiyo ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Yusuph Kisare, Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo, Juma Chagonja na Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo, Onesmo Laizer.

Prof. Ndalichako alizitaja baadhi ya sababu za kufukuzwa na kusimamishwa kazi kwa watumishi hao kuwa ni kufanya malipo yasiyo sahihi kwa baadhi ya wanafunzi wanaosoma ndani na nje ya nchi pamoja na udhaifu uliobainika katika mifuko ya fedha.

Wakati Prof. Ndalichako akichukua hatua hiyo, Takukuru nayo imekiri inaichunguza taasisi hiyo yenye jukumu la kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kusimamia urejeshaji wa mikopo hiyo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Nipashe ilimtafuta jijini Dar es Salaam Ofisa Uhusiano na Habari wa Takukuru Makao Makuu, Mussa Misalaba, ambaye alikiri kuwa wanaichunguza taasisi hiyo kutokana na tuhuma mbalimbali za rushwa na ufisadi zinazowakabili vigogo na maofisa wake.

"Si hilo tu (la posho za mabilioni ya shilingi), tuna mambo mengi ambayo Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu tunaichunguza. Wana tuhuma nyingi ambazo tunazifanyia kazi ili wahusika wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa," alisema Misalaba.

Hata hivyo, Misalaba hakuwa tayari kuziweka wazi tuhuma zingine ambazo vigogo na maofisa wa HESLB wanachunguzwa nazo.

Lakini habari za uhakika ambazo Nipashe inazo, Takukuru inachunguza pia HESLB kwa malipo ya mikopo kwa wanafunzi hewa na ulipaji wa mikopo mpaka minne kwa mwanafunzi mmoja.