Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Zuberi Kabwe amefunguka na kusema kwamba chama chao siyo mawakala wa polisi hivyo hawawezi kwenda nchi nzima kuwakusanya wajumbe wa chama hicho na kuwapeleka polisi kama agizo la Polisi kanda maalumu lilivyoagiza jana.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya kitengo cha upelelezi wa makosa ya kifedha kilichopo Kamata, Kariakoo jijini Dar es Salaam, Zitto amesema kwamba suala la polisi kutaka kuihoji kamati kuu ya ACT-Wazalendo hakiwezekani kwani hawana uwezo wa kuhoji ogani za chama kama Kamati Kuu.
Zitto ameweka wazi kwamba kwa kuwa jeshi hilo halina uwezo huo hivyo kama walivyoeleza jana katika mkutano wao na waandishi wa habari wamewakilishwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Yeremia Maganja na Katibu Mkuu Doroth Semu.
"Polisi hawana uwezo wa kuihoji kamati kuu, ndiyo maana mwenyekiti na katibu mkuu wapo hapa wanaendelea na mahojiano... huwezi kuwaita wajumbe wote wa kamati kuu. Kwa kuwa mtendaji wa chama ni Mwenyekiti na mwenye Mamlaka ya kuisemea chama ni Katibu Mkuu ndiyo maana wamefika," amesema.
Ameeongeza "Tumewaaambia sisi siyo mawakala wa polisi wa kuzunguka nchi nzima kwa ajili ya kwenda kuwakusanya wajumbe wa Kamati kuu ili kuwaleta polisi".