Rais John Magufuli ameagiza mamlaka zinazohusika na masuala ya mazingira kuacha kuwabughudhi wananchi wanaolima pembezoni mwa mito.
Amesema busara itumike wakati wa utekelezaji wa sheria ya mazingira inayozuia shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka kwenye chanzo cha maji ili kuwaondolea kero wakulima wanaojitafutia chakula na kipato cha kawaida kwa ajili ya familia zao.
“Ni vyema utekelezaji wa sheria ya mazingira ya mita 60 ilenge zaidi kubana wanaotumia maeneo ya maziwa na bahari na si wananchi wanaolima mazao ya chakula ya muda mfupi kando mwa mito,” ameagiza.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mwananchi aliyejitambulisha kwa jina moja la Roshi, mkazi wa Kyaka wilayani Missenyi aliyedai kuwa mazao ya chakula yaliyokuwa kwenye shamba lake lililopo kando mwa mto yalifyekwa na watu wa mazingira kwa madai kuwa yalilimwa ndani ya mita 60.
“Mheshimiwa Rais, wakati wewe unatusisitizia wananchi tufanye kazi, watu wa mazingira wanafyeka mazao yetu tunayolima kwenye mashamba yetu yaliyoko kando mwa mto,” alilalamika Roshi.
Akihutubia wananchi wa Wilaya ya Karagwe jana Jumanne Novemba 7,2017 muda mfupi kabla ya kuzindua barabara ya Kyaka-Bugene yenye urefu wa kilomita 59, iliyojengwa kwa kiwango cha lami, Rais Magufuli alisema tangu alipoanza ziara mkoani Kagera juzi Novemba 6,2017 amepokea malalamiko mengi ya wananchi walioharibiwa mazao kando mwa Mto Kagera kwa madai kuwa wamevamia vyanzo vya maji na kuagiza wasibughudhiwe kwa sababu wanatekeleza kauli mbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu’.
Kuhusu wananchi wanaodaiwa kuvamia vyanzo vya maji, Rais ameagiza watu zaidi ya 200 wanaodaiwa kuvamia vyanzo vya maji watafutiwe maeneo mengine kwa sababu ni kosa la viongozi na mamlaka husika zilizozembea kuwazuia mapema kuingia maeneo hayo.
“Bila kutumia busara tunaweza kukuta kila Mtanzania hana sehemu ya kuishi. Viongozi lazima tutumie busara kuepusha matatizo kwa wananchi,’’ alisema Rais Magufuli.