Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita amekanusha uvumi unaomhusisha na mipango ya kujiondoa katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mwita amesema lengo la uzushi huo ni kumchafua hasa kutokana na staili yake ya kazi ya kushirikiana na serikali badala ya kupambana katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za kimeya.
Akisisitiza historia na utamaduni wa Mkurya ni kukataa kuwa msaliti akasema: “Naomba ifahamike kuwa hakuna Mkurya ambaye aliwahi kuwa msaliti katika nafasi yoyote ambayo aliwahi kuwa nayo. Kutokana na historia hiyo, naomba niaminike na wanachama na wananchi wote kuwa haitakuja kutokea Mkurya mimi nikakisaliti chama changu.
“Na kama itakuja kutokea nikafanya hivyo ninaweza kuhatarisha maisha yangu, familia yangu, na hivyo kujikuta nikiingia kwenye matatizo makubwa ambayo kimsingi siyo mazuri. Mama yangu ni mjane, kama itafanya hivyo Chadema wote Mkoa wa Mara hawawezi kuwaacha ndugu zangu salama”.
Meya huyo amesema hajawahi kudhani wala kufikiria kuhama Chadema na kwenda kwenye chama chochote cha siasa kwani ametoka nacho mbali tangu mwaka 2004 kwa kukijenga chama hicho kwa gharama zake mwenyewe ambapo anatambua kuwa chama kimemheshimu kwa kumpa nafasi ya umeya hivyo haoni sababu ya kuondoka kwani ana nia ya kuwatumikia wananchi.
“Kukaa kwangu kimya, kutofanya siasa za kiharakati ndani ya Jiji la Dar es Salaam haimanishi kwamba niko upande wowote ama kukihujumu chama changu. Ila huu ni mfumo ambao nimeuchagua na kujijengea kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na si kufanya harakati za kisiasa kwa kuwa nina nia ya kufanya maendeleo ndani ya jiji la Dar es Salaam.