#MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Mkoani Mara Mh, Isack Mahela Kabugu Amefanya ziara katika kata mbili za Mugeta na Hunyari na kujionea uharibifu Mkubwa wa mazingira uliosababishwa na uchomaji wa mkaa, ufyatuaji wa matofari pamoja na utengenezaji wa zizi ya mifugo.
Akiwa katika kijiji cha Kyandege kata ya Mugeta akiongozana na kamati yake ya fedha,uongozi na mipango mwenyekiti huyo ameshuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira unaodaiwa kufanywa na vijiji viwili vya Kyandege na tingirima katika eneo tengefu la kijiji cha kyandege kwa ajili ya malisho ya mifugo.
Akiwahoji viongozi wa kijiji cha Kyandege kwanini uharibifu huo unafanyika ilhali wapo, kaimu mtendaji wa kijiji hicho bwana Daudi Machota amesema kuwa hali hiyo imetokana na mgogoro wa mpaka uliopo baina ya kyandege na tindirima linalopelekea eneo hilo la malisho ya mifugo maarufu kama shamba la bibi kuharibiwa na wakazi wa vijiji vyote viwili.
Hata hivyo mwenyekiti wa halmashauri wa wilaya mh, Kabugu amewaagiza viongozi wa vijiji hivyo ]Kyandege na tingirima] kusimamia kikamilifu eneo hilo na kusitokee tena suala la ukataji miti kwani kinyume na maagizo hayo viongozi wa serikali ya vijiji hivyo watachukuliwa hatua kali.
Aidha akiwa katika kijiji cha Sarakwa kata ya Hunyari Mwenyekiti wa wilaya amekamata Magunia/mifuko 135 ya mkaa yaliyokuwa yanatarajiwa kusafirishwa kwenda Mkoani mwanza kinyume na taratibu.