IKU tano baada ya mwanaye ambaye ni staa wa Bongo Movies, Elizabeth Michael ‘Lulu’ mama yake mzazi, Lucresia Karugila, kwa mara ya kwanza amefunguka baada ya mtoto wake huyo kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela kwa kosa la kumuua bila kukusudia staa mwenzake, Steven Kanumba aliyekuwa pia mwandani wake.
Awali, kulienea lawama nyingi mitandaoni baada ya Lulu kuhukumiwa kuwa huenda kuna mahali wazazi walikosea malezi ndiyo sababu ya mtoto wao huyo kujihusisha na masuala ya kimapenzi akiwa na umri wa chini ya miaka 18 ambao hakubaliki.
Kufuatia hali hiyo, Ijumaa Wikienda lilimtafuta mama Lulu ili kujua mtazamo wake juu ya mwanaye kwenda jela na madai ya mitandaoni ndipo akafunguka mazito. Mama Lulu aliliambia gazeti hili kuwa, kwa sasa hapendi kuzungumza hovyo na watu na anahitaji muda mwingi wa kupumzika kwa kuwa hayuko vizuri. “Nafikiri kwa kipindi hiki nahitaji zaidi kupumzika kwa muda mwingi na sipendi kuzungumza hovyohovyo, siko vizuri kabisa,” alisema mama Lulu kwa sauti ya unyonge.
Akiendelea kuzungumza, mama huyo alisema kuwa, tangu apate majanga ya mtoto wake huyo hadi kwenda jela hayupo vizuri na wala hapendi kuongea kwa sababu hajisikii kufanya hivyo kwani anahisi anaiona dunia chungu. “Najua watu watanishangaa sana, lakini ndiyo nimeamua kuwa hivyo, siko sawa na sijisikii vizuri kabisa. “Sidhani kama kuna mzazi yeyote anaweza kupata usingizi wakati mwanaye yupo kwenye mateso kama ilivyokuwa zamani, kiukweli ninaumia sana,” alisema mama Lulu.
DAKTARI NAYE ANENA!
Naye daktari wa magonjwa ya binadamu, Dk Godfrey Chale, akizungumzia hali ya Lulu baada ya hukumu hiyo alisema kuwa, kuna magonjwa ambayo huweza kumpata mtu mwenye matatizo ya kimaisha ikiwemo kufungwa jela ikiwa ni pamoja na kuwa kichaa kutokana na msongo.
Dk Chale alisema mara nyingi watu ambao hupatwa na majanga makubwa kama la Lulu, huwa kwenye uwezekano mkubwa wa kukumbwa na msongo ambao husababisha mpangilio mbovu wa homoni kiutendaji na mhusika kuchanganyikiwa endapo atashindwa kukubaliana na mazingira ya tatizo.
Alisema kuchanganyikiwa kwa watu wenye matatizo kama ya Lulu, hutokana na kuzidiwa na huzuni na mgandamizo wa hisia (depression) hivyo kushindwa kabisa kuzuia mfumo wa kufikiri na kutafakari na ndiyo maana unakuta mtu anaongea peke yake au kufanya vitendo vya ajabu kama kuokota vitu mbalimbali kama sehemu ya kujifariji na hapo ndipo tatizo la kuchanganyikiwa huanzia.
Tatizo kubwa jingine ambalo linaweza kumpata Lulu ni kupoteza popularity momentum (nguvu ya umaarufu) na kushuka kwa uchumi atakapomaliza kifungo kwani kwa kipindi ambacho yuko jela atapoteza mikataba yake ya kikazi kama matangazo na uigizaji, vitega uchumi ambavyo vilikuwa vikimuingizia kipato cha kuyaendesha maisha yake
Chanzo : Global Publishers