SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 8 Septemba 2017

T media news

Serikali yatenga Tsh bilioni 1 za mpango wa lishe 2017/18

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo  amesema kuwa   TAMISEMI imetenga bajeti ya  Shilingi Bilioni 1 katika mpango wa lishe wa mwaka 2017/18 wenye lengo la  kupeleka agenda ya lishe kitaifa na kutokomeza  udumavu na utapia mlo nchini.

Mhe. Jafo alisema hayo    jana  kwenye  mkutano  wa nne wa wadau wa sekta ya lishe katika kufanya mapitio ya mpango jumuishi wa lishe 2016/17- 2020/2021 wenye   kauli mbiu ya lishe bora ni msingi wa maendeleo ya viwanda nchini Tanzania  ,   uliofanyika  katika ukumbi wa mikutano Hazina  Mjini Dodoma.

Alisema kuwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI)

Imepewa jukumu la kuratibu mpango wa lishe katika ngazi za Mkoa na Wilaya hivyo mpango huo utatekelezeka kwa kina na uweledi mkubwa katika kuboresha lishe nchini  kupitia dhana ya ugatuaji wa madaraka.

“ Tumejielekeza  vya kutosha katika kuboresha afya ya kila  mtoto,  bajeti ya awali ilikuwa shilingi 500 kwa kila mtoto chini ya miaka 5 lakini  katika bajeti ya sasa 2017/18  TAMISEMI imetenga bajeti ya elfu moja kwa kila mtoto na kuweka jumla ya  Shilingi  bilioni 1 “

Aidha alisema ni wajibu wa kila  Mkuu  wa  Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanasimamia utekelezaji  wa afua zilizoanishwa katika mpango  jumuishi wa utekelezaji wa masuala ya lishe  ili kuboresha afya na kuendeleza agenda ya lishe katika     kuleta maendeleo  ya Taifa kwa ujumla.


Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kasim Majaliwa akimkabidhi Naibu Waziri wa TAMISEMI  Mh. Profesa  Seleman Jafo mpango mpango jumuishi wa lishe 2016/17- 2020/2021   uliofanyika  katika ukumbi wa mikutano Hazina  Mjini Dodoma.

Aliongeza   kuwa  Taifa  linahitaji  watu wenye afya bora ili waweze kuchangia  katika  kuleta maendeleo  nchini  ,  mpango huu  jumuishi wa lishe 2016/17- 2020/2021 una lengo la   kutokomeza utapia mlo na boresha afya  ya mtoto hivyo ni wito wa kila mdau wa afya  kuhahakisha anasimamia kikamilifu  utekelezaji wa mpango huu.

Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kasim Majaliwa alisema kuwa Serikali imejipanga vya kutosha katika kutokomeza utapia mlo nchini hivyo  aliwataka wadau kutoa elimu sahihi ya lishe  na kulipa kipaumbele suala zima la lishe kwa kubuni  sera  na mikakati bora ya kilimo na lishe.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) Bi. Joseline Kaganda alisema kuwa ili kutokomeza utapia mlo nchini  lazima kuwepo na mpango thabiti wa kupambana na chanagamoto hii  pamoja na ushirikiano kati ya Serikali na wadau  wa lishe.

Naye Mkurugenzi wa USAID na mwakilishi wa  Msukumo mpya katika masuala ya lishe  (SUN-NETWORK) Bw. Andrew Karas  amesema kuwa ushirikishwaji wa wananchi ,wadau na Serikali ni muhimu mno katika kutokomeza utapia mlo Tanzania hivyo ni lazima kuimarisha  mahusiano na mifumo iliyopo ili kufikisha huduma kwenye maeneo yaliyo na upungufu.

Mkutano  wa nne wa wadau wa sekta ya lishe katika kufanya mapitio ya mpango jumuishi wa lishe 2016/17- 2020/2021 utakaodumu  kwa siku tatu    katika ukumbi wa mikutano Hazina  Mjini Dodoma   umehudhuriwa na  Maafisa lishe  wa Mikoa na Wilaya nchini,Asasi na mashirika ya kiraia yanayotekeleza afua za lishe,sekta binafsi na Wizara mtambuka pamoja na wadau mbalimbali  wa maendeleo nchini  kwa siku tatu .