SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 20 Septemba 2017

T media news

Rais Museveni aagiza uchunguzi Ufanyike Kubaini chanzo cha ajali iliyoua Watanzania 13

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema upelelezi kubaini sababu za ajali iliyosababisha vifo vya Watanzania 13 waliokuwa wakitoka harusini nchini humo unaendelea.

Waziri wa Ofisi ya Rais anayeshughulikia Jiji la Kampala, Bety Kamya akisoma salamu za rambirambi kutoka kwa Rais Museveni amesema licha ya kutoa pole kwa familia, kiongozi huyo ameagiza uchunguzi wa sababu za ajali ufanyike.

Amesema pia amewapongeza maharusi, Dk Aneth na Dk Trease Ibingira na amewatakiwa maisha mema ya ndoa.

Mbali ya hilo, amesema anawaombea ili kukabiliana na kipindi kigumu walichonacho.

Amesema Rais anawashukuru Watanzania kwa kuwa wavumilivu katika kipindi kigumu cha kupoteza wapendwa wao.

"Nakabidhi vyeti hivi vya vifo vya ndugu zetu 13 nawapa pole sana," amesema Waziri Kamya akimkabidhi vyeti hivyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki.

Waziri Kairuki amesema Rais John Magufuli amepokea taarifa ya vifo hivyo kwa mshtuko na alitoa maelekezo ya kupokewa miili hiyo, kuhifadhiwa kwenye Hospitali ya Jeshi Lugalo, kuagiwa hapo na kusafirishwa kwa maziko.

Amesema maagizo hayo wanaendelea kuyatekeleza ikiwa ni pamoja na kutoa magari kwa ajili ya kusafirisha miili hiyo.

Waziri Kairuki amesema kwa namna isiyo katika wakati wa kawaida, anawapongeza maharusi na kuwatakia maisha mema.

"Haya ni mapenzi ya Mungu, hili lisiwanyong'onyeshe maharusi," amesema Kairuki.

Ameishukuru Serikali ya Uganda kwa kukodi ndege kuirudisha nyumbani miili hiyo.