Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru vigogo watatu wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka(DART), akiwemo mtendaji mkuu wa mradi huo, Asteria Mlambo na mwenzao.
Akitoa hukumu hiyo leo Jumatano ni Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage amesema baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi 10 wa upande wa mashtaka, vielelezo na ushahidi wa upande wa utetezi ameona upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka yote yaliyokuwa yakiwakabili vigogo hao pasipo kuacha shaka.
Mbali na Mlambo wengine walioachiwa huru ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Evodius Katale, Mwanasheria Mkuu wa DART, Francis Kugesha na mkurugenzi wa kampuni ya Yukan, Yuda Mwakatobe.
Washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kusababisha hasara ya Sh 83.5 milioni.
Katika kesi hiyo ilidaiwa kuwa Septemba Mosi na Oktoba Mosi, mwaka 2013 maeneo ya Kinondoni Dar es Salaam, Mlambo, Katale na Kugesha wakiwa wafanyakazi wa mradi huo, walishindwa kutekeleza majukumu yao vizuri na kuisababishia Serikali hasara ya Sh 83.5 milioni.