Ligi kuu Tanzania bara itaendelea tena Alhamisi ya September 21, 2017 ambapo uwanja wa CCM Kirumba Mwanza kutakuwa na shughuli pevu kwenye mchezo kati ya Mbao FC vs Simba, mechi inatarajiwa kuwa ya kuvutia kutokana na mambo kadhaa yanayozihusu hizo timu mbili.
shaffihDauda.co.tz imeangalia baadhi ya mambo yanayoufanya mchezo huo kuwa wenye upinzani na kuvutia kwa mashabiki kutazama
Historia Mbao vs Simba
Timu hizi zimekutana mara tatu, mechi mbili kati ya hizo ni ligi kuu huku mchezo mwingine ukiwa ni wa fainali ya FA Cup 2017. Simba imeshinda mechi zote tatu, mbali ya Simba kushinda mechi hizo, upinzani waliokutana nao haukuwa wa kitoto.
October 10, 2016 Simba ilishinda 1-0 dhidi ya Mbao kwenye uwanja wa Uhuru, Dar. Goli la dakika za lala salama likaipa Simba pointi tatu, April 10, 2017 Mbao wakapoteza nyumbani baada ya kufungwa bao 3-2 kwenye mechi ambayo ilikuwa ni ya aina yake. Simba walitoka nyuma baada ya kutangulia kufungwa 2-0 wakasawazisha magoli yote na kuongeza bao jingine la ushindi.
May 27, 2017 Simba wakaifunga tena Mbao 2-1 kwenye mechi ya fainali ya FA Cup iliyochezwa kwa dakika 120 kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma na Simba wakafanikiwa kushinda kombe hilo.
Matokeo Simba, Mbao, msimu huu
Tayari kila timu imeshacheza mechi tatu za ligi hadi sasa, Mbao imeshinda mechi moja na kupoteza mechi mbili (Kagera Sugar 0-1 Mbao, Singida United 2-1 Mbao, Mtibwa Sugar 2-1 Mbao) Mbao imefanikiwa kufunga goli katika mechi zote walizocheza kwa maana hiyo wana pointi tatu na magoli matatu katika mechi tatu walizocheza.
Mbao imecheza mechi zote tatu ugenini, mchezo wao wa nne dhiid ya Simba watakuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani CCM Kirumba, Mwanza.
Simba wao bado hawajapoteza mechi katika mechi tatu walizocheza, wameshinda mechi mbili na kutoka sare mchezo mmoja (Simba 7-0 Ruvu Shooting, Azam 0-0 Simba, Simba 3-0 Mwadui) wanapointi saba na magoli 10 ikiwa wao hawajaruhusu goli hadi sasa.
Simba watakuwa wakicheza mechi yao ya kwanza nje ya Dar baada ya kucheza mechi zao tatu jiji Dar es Salaam, mechi mbili kati ya hizo wamecheza nyumbani (Uhuru) huku mechi moja wakicheza ugenini (Azam Complex).
Vikosi
Simba ina kikosi cha wachezaji wengi wenye uzoefu kwenye soka ikiwa ni pamoja na VPL (Bocco, Okwi, Manula, Nyoni, Mkude) ni baadhi ya wachezaji waliocheza mechi nyingi za VPL huku kikosi chao kikiwa na wachezaji saba wa kimataifa ambao wengi kati ya hao wanaanza kwenye kikosi cha kwanza (Okwi, Mwanjale, Kotei, Niyonzima).
Kwa upande wa kikosi cha Mbao wao timu yao imesheheni vijana wengi ambao wengi wao ndio wanacheza ligi kuu kwa mara ya kwanza, kocha wa Mbao Ettiene anaendelea kuwajenga siku hadi siku na ameshasikika akisema licha ya kupoteza mechi zao mbili zilizopita kiufundi amefurahia vijana wake walivyocheza.
Mbao hawana mchezaji hata mmoja kutoka nje ya nchi, wachezaji wote ni wazaliwa wa mikoa tofauti ya Tanzania.
Wanakutana na Simba ambayo imechomoa wachezaji kadhaa kutoka Mbao (Emanuel Mseja, Jamal Mwambeleko) ni wachezaji walioitumikia Mbao msimu uliopita hivyo watakuwa wakirejea kwenye uwanja wao wa zamani.
Nafasi kwenye msimamo wa ligi
Simba inashika nafasi ya pili kwenye msimmao ikiwa na pointi saba baada ya mechi tatu wakati Mbao wenyewe wapo katika nafasi ya 10 wakiwa na pointi tatu baada ya mechi tatu. Ikiwa Simba watashinda watafikisha pointi 10 na kuongoza ligi juu ya Mtibwa Sugar lakini Simba watakuwa mbele kwa idadi ya mechi kuliko Mtibwa yenye pointi tisa hadi sasa baa kushinda mechi zao tatu.
Endapo Mbao watashinda watafikisha pointi saba na watapanda kwenye msimamo hadi nafasi ya nne au ya tatu (inategemea na idadi ya magoli watakayoshinda).
Ikiwa timu hizo zitatoka sare, Simba itafikisha pointi nane na kusalia kwenye nafasi yake ya pili wakati Mbao watafikisha pointi nne na kuwa sawa na Ndanda wanaoshika nafasi ya tisa kwenye msimamo.
Mtazamo wangu
Simba inaidara hatari ya ushambuliaji, inashambulia kutoka katika kila pembe na inafunga magoli ya kutosha ukilinganisha na timu nyingine lakini ngome yao ya ulinzi imekuwa ngumu kupitika ikiwa haijaruhusu goli hata moja hadi sasa wanakutana na Mbao timu yenye vijana wengi wasio na majina makubwa wanaocheza kwa kujitoa na kitimu zaidi kuliko kumtegemea mchezaji mmoja.
Atakaekuwa amejipanga vizuri kiufundi, kimbinu na kisaikolojia kati ya Ettiene na Omog timu yake itaweza kupata matokeo.