SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 19 Septemba 2017

T media news

Kocha wa Mbao kazungumza mambo matatu, kawashika sikio watu wa Mwanza

Kocha mkuu wa Mbao FC Ettiene alikuwa mgeni mwalikwa kwenye kipindi cha Sports Bar cha Clouds TV kilichoruka Live kutoka Rock City Mall jijini Mwanza ambapo pamoja na mambo mengine, ilichezeshwa draw ya kupanga makundi ya Ndondo Cup 2017 mkoani Mwanza.

Ettiene alizungumzia mambo kadhaa yanayoihusu timu yake anayoiongoza kwa msimu wa pili ikiwa ligi kuu Tanzania bara ligi yenye jumla ya timu 16.

Mechi tatu pointi tatu

Tangu kuanza kwa ligi msimu mpya, Mbao tayari imeshacheza mechi tatu na kuambulia pointi tatu katika mechi hizo. Walishinda 1-0 mechi yao ya ufunguzi ugenini walipocheza dhidi ya Kagera Sugar lakini mechi mbili nyingine wakapoteza.

“Licha kutofanya vizuri kwenye mechi mbili zilizopita, kiufundi wachezaji wamekua wakiimarika mechi hadi mechi”-Ettiene.

“Jambo zuri ni kwamba tumeweza kufunga goli katika kila mechi tuliyocheza.”

Wachezaji waliopo Mbao ni bora kuliko walioondoka

Mbao ni timu inayoamini katika vijana, ndio maana si jambo la kushangaza sana kuona inawachezaji wengi vijana ambao hawajawahi kucheza ligi, ndio wanaanza kuonekana wakiwa Mbao.

Msimu uliopita wachezaji wengi wa timu hii walifanya vizuri licha ya ugeni wao kwenye ligi, mwisho wa msimu vilabu vikubwa vya Bongo vikaanza kupambana kusajili wachezaji kutoka Mbao.

Salmini Hoza, Pius Buswita, Jamal Mwambeleko, Emanuel Mseja, Benedict Haule ni baadhi ya wachezaji walioondoka kwenye kikosi cha Ettiene na kwenda kutafuta maisha kwenye vilabu vya Simba, Yanga na Azam.

“Wachezaji wakiondoka wanatoa nafasi kwa wengine nao kuonekana na kusogea juu. Wachezaji waliopo sasa Mbao ni bora zaidi kuliko walioondoka.”

“Sasa hivi wachezaji wamepewa mikataba mirefu ili hata wakiondoke isiwe bure klabu nayo ipate chochote.”

Mwanza zipendeni timu zenu 

Tanzania bado inaathiriwa na mapenzi kwa vilabu vya Simba na Yanga, vialabu hivi viwili kila vinapocheza lazima vitapata mashabiki, Ettiene amewaomba wadau wa Mwanza mbali na mapenzi yao kwa vilabu hivyo wasiache kutoa ushirikiano kwa timu zao za nyumbani.

“Mbao, Toto Africans, Alliance na Pamba ni vilabu vya Mwanza vinahitaji ushirikiano kutoka kwa watu wa hapa, endapo vilabu vyote vitakuwa ligi kuu inamaana Simba na Yanga zitakuja Mwanza mara nne. Mtaziona Simba na Yanga zikicheza hapa na vilabu vyenu itasadia pia uchumi wa Mwanza kupanda kwa sababu watu watauza vyakula, vinywaji, hoteli, usafiri na kila kitu kitakuwa vizuri.”