Mbunge wa Singida Kaskazini Lazaro Nyalandu ambaye amekuwa akifuatilia kwa ukaribu matibabu ya mbunge mwenzake wa Singida Mashariki Tundu Lissu, ameweka wazi kwamba jitihada za kumpeleka Lissu Marekani kutibiwa kwa sasa zimegonga mwamba.
Lazaro Nyalandu ametoa taarifa hiyo kwenye ukurasa wake wa facebook ambapo amendika ujumbe kuhusu kauli ya madaktari wanaomtibu Tundu Lissu jijini Nairobi Kenya, na kueleza kwamba madaktari hao wamesema hawawezi kuruhusu Tundu Lissu asafirishwe kupelekwa Marekani kutokana na hali yake jinsi ilivyo.
“Kwa sasa mipango ya kumsafirisha Mheshimiwa Tundu Lissu nje itasimama kutokana na ushauri wa madaktari wa hospitali ya Nairobi, ili kuruhusu kukamilishiwa huduma za tiba ambazo tayari ameanzishiwa hadi hapo itakavyoshauriwa au vinginevyo, ama endapo kutatokea umuhimu wa kufanya hivyo katika siku zijazo”, ameandika Lazaro Nyalandu.
Hapo jana Lazaro Nyalandu alitoa taarifa kwamba wanafanya jitihada za kumpeleka Tundu Lissu Marekani kwa ajili ya matibabu zaidi, huku wakisubiria ripoti ya madaktari wa hospitali ya Nairobi ambako mbunge huyo anatibiwa, na ndipo ilipokuja taarifa hiyo kwamba haitowezekana kumsafirisha kwa sasa.
Ikumbukwe kuwa Mbunge Tundu Lissu alipigwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 mjini Dodoma majira ya mchana, na usiku wa siku hiyo hiyo alikimbizwa jijini Nairobi kwa ajili ya matibabu zaidi, kutokana na hali yake kutokuwa nzuri.
==>>Huu ni ujumbe alioundika Lazaro Nyalandu
TUNAFAHAMU kwamba, tangu Alhamisi, Septemba 7, siku ambayo Mh #TunduLissu, Mb., (Singida Mashariki-CHADEMA) alishambuliwa kwa kupigwa risasi mjini DODOMA, Watanzania wengi wamesononeshwa na kulia sana, na kubwa zaidi, WOTE wameungana katika kuomba Sala na Dua kwa ajili ya Mh #TunduLissu, ili mkono wa Mkombozi, aliye MUNGU wetu, upate kumgusa tena na kumponya dhidi ya majeraha, maumivu na mateso anayoyapitia.
MAPEMA leo, baada ya kutembelea #NairobiHospital asubuhi, nimefanya mazungumzo mchana wa leo na Mh #FreemanMbowe, ambapo kwa pamoja tumeelezwa kuwa MADAKTARI #NairobiHospital wameendelea na kumtibu Mh #TunduLissu, ikiwa ni pamoja na kuanza upasuaji, na huduma zingine za Kitabibu walizomwanzishia tangu awasili Nairobi siku ya Alhamisi, Septemba 7. IMEELEZWA vilevile kuwa kwa sasa Mh #TunduLissu ataendelea na TIBA hospitalini hapo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa hali yake bado ni "Critical but stable", na KWAMBA mwili wake unaendelea kuitikia vema matibabu lukuki anayofanyiwa kwa wakati mmoja.
KWA SASA, mipango ya kumsafirisha Mh #TunduLissu NJE itasimama, kutokana na ushauri wa MADAKTARI #NairobiHospital, ili kuruhusu kukamilishiwa huduma za TIBA ambazo tayari ameanzishiwa, hadi hapo itakavyoshauriwa vinginevyo, ama endapo kutatokea umuhimu wa kufanya hivyo katika SIKU zijazo.
AIDHA, SOTE tuzidi KUMWOMBEA MUNGU na kushiriki katika CHANGIZO za kusaidia gharama za matibabu yake.
NI DHAHIRI kwamba Wana Singida, na Watanzania WOTE tumeumia, tumekwazwa, na tumesononeshwa sana kwa uonevu na dhuluma aliyotendewa ndugu yetu Mh #TunduLissu. Kitendo hiki hakikubaliki mbele za MUNGU na mbele za wanadamu.
Tunaiomba Serikali yetu iendeleze juhudi zake na kuchukua hatua za haraka kuwasaka, kuwakamata, na kuwatia mbaroni watu wote waliohusika kupanga na kutekeleza shambulio hili la kigaidi dhidi ya Mh #TunduLissu. Aidha, shambulio hilo walilolifanya watu wasiojulikana limedhalilisha taifa, na kudhoofisha taswira ya kukomaa kwa demokrasia inayoruhusu kuvumiliana na kuheshimiana licha ya tofauti zetu za kiitikadi na mitazamo ya kisiasa.
HALIKADHALIKA, kwetu sote kama TAIFA, huu ni wakati wa Watanzania wote kuwa wamoja, bila kujali tofauti zetu za kiitikadi, kidini, wala kikabila, tuungane na kulaani kitendo hiki na vitendo vyote vya uonevu na kuumizana. TANGU zamani, IMEANDIKWA: Haki HUINUA Taifa.
Lazaro S Nyalandu, Mb.
Singida Kaskazini-CCM
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (TAIFA)